Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuchukua hatua za makusudi ikiwemo kuwavua nyadhifa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Uzalishaji, Mhandisi Abdallah Ikwasa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji, Mhandisi Kahitwa Bashaija; kutokana na suala la kukatika umeme sehemu kubwa ya nchi mara kadhaa sasa.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhusu hatua za kuchukua kutokana na suala la kukatika umeme sehemu kubwa ya nchi mara kadhaa. Waziri alikutana na Bodi hiyo Desemba 15, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma. Kulia kwa Waziri ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua.

Alitoa maagizo hayo Jumamosi Desemba 15, mwaka huu alipokutana kwa dharura na wajumbe wa Bodi hiyo Makao Makuu ya Wizara jijiji Dodoma.

Akizungumzia sababu za kutaka wakurugenzi hao wawajibishwe, Waziri Kalemani alisema ni kutokana na tatizo la kukosekana kwa umeme sehemu kubwa ya nchi mara nne na kwa kipindi cha muda mrefu unaofikia nusu saa, kwa sababu ambazo zimekuwa zikielezwa kuwa ni kutoka kwa Gridi ya Taifa, wakati nchi ina ziada ya umeme inayofikia wastani wa megawati 250.

Akifafanua zaidi, alisema kutokea kwa tatizo hilo kunamaanisha kuna uzembe katika usimamizi au kutokufuatilia maelekezo ya Serikali, au kunaweza kuwepo na hujuma kwa baadhi ya watumishi wasiokuwa wazalendo.

“Nchi inapokuwa gizani hata kwa sekunde moja, maana yake hakuna usalama. Aidha, hakuna sababu ya wananchi kukosa umeme katika mazingira ambapo kuna umeme wa ziada.”

Katika maagizo yake kwa Bodi, mbali na kutaka Wakurugenzi husika wawajibishwe, aliagiza pia wachunguzwe ikiwa ni pamoja na waliohusika kwa namna moja ama nyingine.

Aidha, aliitaka Bodi kuunda Timu mahsusi kuanzia siku hiyo (Desemba 15), ili ichunguze na kufuatilia suala hilo, ikihusisha tasnia na taasisi mbalimbali, zaidi ya TANESCO.

“Ndani ya siku saba nipate matokeo ya nini chanzo chat atizo hilo ili lisijirudie kabisa,” alisisitiza.

Waziri pia aliitaka Bodi kuhakikisha maeneo yote ya mijini ambayo hayana umeme kwas asa; yakisubiri kuunganishwa na huduma hiyo kupitia shirika hilo, yaanze kuunganishwa kuanzia siku hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Alisema yako maeneo ya mijini ambayo yanahitaji kuunganishiwa umeme na yamekaa kwa muda mrefu huku yakiwa ndani ya Mpango wa shirika na tayari pesa ilikwishatolewa kwa kila Mkoa.

Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) alipokutana nao na kuwapa maagizo kuhusu hatua za kuchukua kutokana na suala la kukatika umeme sehemu kubwa ya nchi mara kadhaa. Waziri alikutana na Bodi hiyo Desemba 15, 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

Vilevile, Waziri Kalemani aliagiza wateja wote nchi nzima ambao wamelipia bili zao, waunganishiwe umeme ifikapo Desemba 31 mwezi huu.

Katika hatua nyingine, Waziri aliitaka Bodi kuchunguza mambo mengine pia kadri itakavyoona inafaa ili kuhakikisha ustahimilivu wa umeme nchini unaendelea kuwepo. “Tuhakikishe maeneo yote nchini hayakatiki umeme pasipo sababu ya msingi.”

Pia, alitaka pindi matengenezo yanapofanyika wananchi wapewe taarifa na wajulishwe muda yatapokamilika.

Sambamba na maagizo hayo, alimtaka pia Mwenyekiti wa Bodi kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watumishi wengine wa Shirika hilo watakaoonesha dalili za kuhujumu miundombinu husika.

Matukio hayo ya kukatika umeme sehemu kubwa ya nchi hivi karibuni yametokea Novemba 28, Novemba 30, Desemba 4 na Desemba 14 mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Hamisi Mwinyimvua na baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya Wizara pia walishiriki mkutano huo wa Waziri na Bodi ya TANESCO.

Na Veronica Simba – Dodoma.

office 365 kaufen