• Atoa maagizo mbalimbali

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua Baraza la Kwanza la  Wizara ya Nishati na kutoa maagizo mbalimbali kwa Watendaji wa Wizara na Taasisi ili  Sekta ya Nishati iendelee kuwa injini katika ukuaji wa uchumi.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akifungua boksi lenye makabrasha ya mkataba wa kuunda Baraza la Wafanyakazi kati ya Wizara ya Nishati na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati.

Dkt. Kalemani amezindua Baraza hilo tarehe 11 Mei, 2018 mkoani Dodoma ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria uzinduzi huo akiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Katibu wa TUGHE mkoa wa Ilala, Tabu Mambo, ambaye alimwakilisha Katibu wa TUGHE Taifa na Katibu wa TUGHE mkoa wa Dodoma, John Mchenya.

Akizungumza na Wajumbe wa Baraza, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na Wajumbe wa TUGHE, Tawi la Wizara ya Nishati, Dkt. Kalemani alisema kuwa, jukumu kuu la Wizara na Taasisi zake ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata nishati ya umeme ya kutosha hivyo wana jukumu la kutafakari namna ya kutekeleza suala hilo.

Dkt. Kalemani, aliwaagiza watendaji wa Wizara na Taaisi kuhakikisha kuwa kunakuwepo na miundombinu ya kutosha ya kusafirisha umeme ili umeme unaozalishwa uweze kuwafikia wananchi kwani kuna sehemu ambazo umeme umekuwa ni mwingi kuliko matumizi ya nishati hiyo.

Aidha, Dkt Kalemani aliwataka watendaji hao kuhakikisha kuwa, wananchi waliolipia huduma ya umeme,  wanaunganishwa na huduma hiyo ndani ya wakati ambao ni siku Saba.

Vilevile Dkt. Kalemani, alisema kuwa, kila mtendaji ana jukumu la kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Kuhusu masuala yanayohusu Watumishi, Dkt Kalemani aliagiza kuwa watumishi wanaokaimu nafasi mbalimbali kwa muda mrefu wathibitishwe katika nafasi hizo ili watumishi hao watekeleze majukumu yao kwa kujiamini na kuwa na ari.

Waziri wa Nishati pia aliagiza kuwa, watumishi wapandishwe madaraja kama inavyostahili ili kuwapa morali ya kufanya kazi, pia motisha na mafunzo sehemu ya kazi yaendelee kutolewa ili kuwajengea uelewa watumishi na hivyo kuleta ufanisi katika Sekta wanayoisimamia.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, pamoja na kupongeza ushirikiano anaopata kutoka kwa Watendaji wa Wizara na Taasisi katika majukumu yake ya kila siku, aliwataka watendaji hao kuhakikisha kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Waziri wa Nishati yanatekelezwa.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua (wa pili kushoto), Katibu wa TUGHE mkoa wa Ilala, Tabu Mambo, ambaye ni mwakilishi wa Katibu wa TUGHE Taifa (wa kwanza kulia), Katibu wa TUGHE mkoa wa Dodoma, John Mchenya (wa kwanza kushoto) na Katibu Mpya wa Baraza la Wafanyakazi, Wizara ya Nishati, Pascal Mduma (wa pili kulia) wakiimba wimbo wa Mshikamano wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati uliofanyika mjini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua alisema kuwa Baraza hilo  la Wafanyakazi ni muhimu kwani pamoja na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Watumishi, pia litajadili utekelezaji wa miradi ya Sekta ya Nishati kwa mwaka 2017/2018 na mipango ya maendeleo kwa mwaka 2018/2019.

Vilevile alisema kuwa, Baraza hilo litajadili Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2017/18 na litapitia Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2018/19.