Benki ya Dunia (WB) imetenga takriban Dola za Marekani bilioni 1.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Nishati nchini Tanzania kwa Mwaka 2017 hadi 2021. Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa kusafirisha umeme kwa Msongo wa kV 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania na Malawi, Bella Bird, alipomtembelea Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani Ofisini kwake jijini Dar es Salaam tarehe 31 Mei, 2018.

Bird alisema kwamba, tayari majadiliano kati ya Wataalamu kutoka serikalini na Benki ya Dunia yamekamilika, ambapo hatua inayofuta ni kujadiliwa na Bodi ya Benki ya Dunia tarehe 18 Juni mwaka huu.

“Kama mradi huu ukipitishwa na Bodi yetu, huu ni mojawapo ya miradi ambayo itatekelezwa na fedha hizo zilizotengwa” alisema Bird.

Aidha, Bird alitoa maelezo kuwa, fedha hiyo iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya nishati nchini itatolewa serikalini kupitia Wizara ya Fedha ikiwa kama mkopo wenye masharti nafuu.

Pia, Bird alieleza umuhimu wa kushirikisha Sekta binafsi katika kuzalisha umeme, ambapo alitoa mfano wa Kenya ambapo sekta binafsi imekuwa na ushiriki mkubwa hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa hali ya upatikanaji wa umeme nchini humo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani aliishukuru Benki ya Dunia kwa jitihada zake inayofanya kufanikisha utekelezaji wa miradi ya nishati nchini Tanzania.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (mbele) akizungumza kati yake na Benki ya Dunia. Wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania na Malawi, Bella Bird na wengine katika picha ni wajumbe kutoka Benki ya Dunia.

Pia Dkt. Kalemani aliishukuru Benki ya Dunia kwa kufanikisha mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kusafirishia umeme kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga ambao ulikamilika mwaka 2016.

Aliongeza kuwa, miradi mingine ambayo Serikali imeiomba  Benki ya Dunia kufadhili ni pamoja na Mradi wa kusafirishia Umeme kutoka Sumbawanga hadi Kigoma kupitia Mpanda wenye kV 400 ambao utaunganishwa hadi Burundi, Mradi wa kuzalisha umeme kutoka Masaka (Uganda) hadi Mwanza (Tanzania) kupitia Bukoba, Mradi wa kuzalisha umeme wa maji Songwe wa MW 180 ambao utekelezaji wake utahusisha nchi mbili ikiwa ni Tanzania na Malawi na Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Ruhuji wa MW 358

Dkt. Kalemani pamoja na mambo mengine alieleza jitihada ambazo wizara inafanya hasa katika suala la kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali (Energy Mix) ambapo alisema kuwa,  Gesi Asilia hadi sasa inachangia zaidi ya asilimia 50 katika umeme unaozalishwa nchini.

“Kuna vyanzo mbalimbali vya nishati kama vile Nishati ya Jua, Upepo, makaa ya mawe katika kuzalisha umeme nchini.” Alisema Dkt. Kalemani.

Aidha, alieleza kuwa Wizara pia imesitisha matumizi ya mitambo ya mafuta kwa asilimia kubwa ili kupunguza gharama katika uzalishaji wa umeme lengo likiwa ni kuwapelekea wananchi umeme wa gharama nafuu.

Na Rhoda James.