Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amesema kuwa, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, vijiji vyote katika Wilaya ya Pangani mkoani Tanga vitakuwa vimeunganishwa na huduma ya umeme.

Aliyasema hayo tarehe 27 Machi, 2018 akiwa katika ziara kukagua utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme vijijini wilayani humo.

Akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah Issa pamoja na uongozi wa Wilaya hiyo, Dkt Kalemani alisema kuwa, ni vijiji vitano tu kati ya vijiji 33 ndivyo havijapata huduma ya umeme wilayani humo hivyo kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo itakamilika mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah Issa, akisoma taarifa ya Wilaya hiyo kwa Waziri wa Nishati, Dkt Medard wakati alipofika wilayani humo kukagua utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini Awamu ya Tatu.

Aidha, alisema kuwa, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme wilayani humo ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme.

Aliongeza kuwa, Serikali kupitia TANESCO itajenga kituo cha kupoza umeme wilayani Pangani ili kuwawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika kwani umeme unaopatikana sasa unatoka katika kituo cha Majani Mapana kilichopo jijini Tanga.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati alizungumza na wananchi wa kijiji cha Mivumoni ambapo aliwaahidi kuwa umeme utawaka wiki ijayo kwani Mkandarasi wa usambazaji wa umeme tayari ameshaanza kazi katika kijiji hicho.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah Issa, pamoja na kupongeza juhudi za usambazaji umeme vijijini katika wilaya hiyo, alimwomba Waziri wa Nishati kushughulikia suala la kukatika mara kwa mara kwa umeme katika wilaya hiyo, suala linalorudisha nyuma shughuli mbalimbali ikiwemo za kiuchumi.

Na Teresia Mhagama, Tanga