Aliyoyasema Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani

Nampongeza Rais, Dkt John Pombe Magufuli kwa kuchukua hatua madhubuti na za ujasiri katika kutekeleza mradi huu ambao ni wa muda mrefu lakini  kwa sasa Serikali imeamua kuutekeleza.

Mradi ulianza kufanyiwa usanifu miaka ya 1970 lakini gharama za utekelezaji zilikuwa kubwa na kwa kipindi hicho umeme uliokuwa ukihitajika ni megawati 100 tu,,, ila kwa leo mahitaji ya umeme ni makubwa, tunahitaji kutekeleza mradi huu sasa na si baadaye.

Mkandarasi wa mradi huu ana majukumu makubwa manne ambayo ni kujenga bwawa kuu lenye uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo bilioni 35, kujenga kituo cha kufua umeme kitakachokuwa na mashine Tisa za kuzalisha umeme wa megawati 235 kila moja hivyo kwa ujumla zitazalisha megawati 2115.

Kazi nyingine za mkandarasi ni kujenga kituo cha kupoza na kukuza umeme cha kV 400 na kujenga njia za kusafirisha umeme utakaoingia katika gridi ya Taifa kwa kutumia njia kuu mbili ambazo ni kutoka eneo la mradi kwenda Chalinze ili kuunganishwa na njia ya kutoka Chalinze kwenda Dodoma na Dar es Salaam.

Njia nyingine ya Umeme ya kV 400 itajengwa kutoka Rufiji kuelekea Kibiti ambapo takribani Vijiji 21 vitafaidika na umeme huo.

Mradi wa umeme wa Rufiji una manufaa mbalimbali ikiwemo, kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya Taifa, kuvutia shughuli za utalii ambazo zitaingiza kipato kwa nchi, maji ya bwawa yataweza kutumika kwa shughuli za umwagiliaji na hivyo kuchochea kilimo cha kisasa, pia Vijiji 37 na vitongoji 142 vinavyopitiwa na mradi vitasambaziwa umeme.

Utekelezaji wa mradi utapelekea kupungua kwa gharama za nishati kwani nchi ambazo zinatumia umeme wa maji kwa wingi gharama zake za umeme zipo chini kuliko zinazotumia vyanzo vingine vya nishati, mfano sisi leo gharama ya umeme ni Dola senti 11 kwa uniti huku Ethiopia ambako wanatumia sana umeme wa maji gharama ni Dola senti 2.4.

Wito wangu kwa wakandarasi ni kutekeleza mradi huu, kwa weledi na ufanisi mkubwa ili ukamilike ndani ya muda uliopangwa na wasiondoke eneo la kazi kwani miundombinu yote wezeshi kama nyumba, maji, umeme na Reli imeshakamilika.

Nampongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati pamoja na wataalam wote waliofanya kazi za maandalizi ya mradi pamoja majadiliano mbalimbali ambayo yamepelekea mradi huu kuanza kutekelezeka.

Aliyoyasema Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu

Ninawaahidi watanzania kuwa, mimi na watendaji wenzangu ndani ya Wizara ya Nishati tutasimamia kikamilifu mradi huu ili uweze kutekelezaka kwa wakati.

Aliyoyasema Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Dkt.Ashatu Kijaji

Wizara ya Fedha imejipanga vizuri katika kuhakikisha kuwa mradi huu wa kihistoria  ndani ya Taifa letu unatekelezeka.

 Dira ya Taifa inaelekeza kuwa mpaka mwaka 2025  tuwe na Tanzania ya kipato cha kati na hili halitawezekana bila kuwa na Tanzania ya Viwanda ambavyo navyo uwepo wake unategemea uwepo wa umeme wa bei nafuu, hivyo mradi huu ni muhimu katika kuhakikisha kuwa Dira hii inatekelezeka.

Aliyoyasema Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu

Wizara ya Maliasili na Utalii imepewa majukumu mawili makubwa ambayo ni kutoa ulinzi kwa wakandarasi na watu wote wanaofanya kazi katika eneo hili na kusafisha beseni litakalotumika kuhifadhi maji yatakayotumika katika mradi huu.

Kwa ujumla tunaendelea kutekeleza vizuri majukumu haya tuliyokabidhiwa na tunaahidi kuwa kwa yote yatakayojitokeza huko mbele tutaendelea kuyatekeleza bila wasiwasi.

Aliyoyasema Makamu wa Rais, Elsewedy Electric, Eng. Wael Hamdy.

Kwa niaba ya Serikali ya Misri, napenda niwahakikishie kuwa tutatekeleza mradi huu kwa ufanisi mkubwa bila kujali changamoto zozote.

Huu si mradi mwepesi kutekeleza lakini kwa sisi kama wahandisi hii ni kazi yetu hivyo tutaitekeleza ipasavyo na huu si mradi wa kwanza kwetu kuutekeleza.

Tunawaahidi kuwa hatutaawangusha, tutakabidhi mradi kama kama yalivyo matarajio yenu na ndani ya wakati uliopangwa.

Na Teresia Mhagama