Zabuni kwa ajili ya mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme wa Megawati 2100 katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji imefunguliwa tarehe 02 Februari, 2018.

Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi kutoka Wizara ya Nishati, Amon MacAchayo (mbele) akizungumza na wawakilishi wa kampuni mbalimbali zilizoomba zabuni kwa ajili ya mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji kwenye ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam tarehe 02 Februari, 2018

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa zabuni hizo kwenye Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi kutoka Wizara ya Nishati, Amon MacAchayo amesema zabuni hiyo ni ya Awamu ya Pili kutokana na kukosekana kwa mshindi katika Awamu ya Kwanza iliyotangazwa mapema mwaka jana.

Alisema kuwa, katika awamu ya kwanza jumla ya kampuni 81 zilinunua nyaraka za Zabuni ambapo nakala moja ilikuwa inauzwa kwa shilingi 200,000 lakini ni kampuni Nne tu zilifanikiwa kurejesha maombi na kuongeza kuwa kampuni zote Nne hazikuwa na  vigezo vinavyohitajika hali iliyopelekea kutangazwa upya kwa zabuni tarehe 19 Desemba, 2017 katika vyombo vya habari  vya ndani na nje ya nchi.

MacAchayo aliongeza kuwa, katika awamu ya Pili kampuni 17 zilijitokeza katika ununuzi wa nyaraka kwa gharama ya shilingi 500,000 kwa kila moja ambapo mpaka siku zinafunguliwa, kampuni Tano ndiyo  zimerejesha nyaraka zenye maombi ya Zabuni.

Sehemu ya wajumbe wakifuatilia zoezi la ufunguaji wa zabuni kwa ajili ya mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji katika kikao hicho.

Alisema hatua inayofanyika kwa sasa ni ufanyaji wa tathmini ya nyaraka za zabuni hiyo na kusisitiza kuwa mara baada ya kukamilika kwa tathmini ya zabuni hizo waombaji wote watajulishwa mshindi na baada ya hapo zitafuata taratibu za mazungumzo, barua na kuandaa mkataba kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi mara moja.

Aliwataka kampuni zilizowasilisha maombi kuwa watulivu wakati zoezi la tathmini likiendelea.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam