Zabuni ya Ujenzi wa Mradi wa kuzalisha Umeme kiasi cha MW 2100 kwa kutumia maporomoko ya maji katika Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) imefunguliwa leo tarehe 27/11/2017 ambapo Kampuni 81 zilijitokeza kununua nyaraka za Zabuni hizo na  kampuni Nne  ndizo  zilizorudisha nyaraka za zabuni husika.

Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati pamoja na watendaji kutoka kampuni mbalimbali zilizonunua zabuni ya Mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge wakiwa katika kikao cha ufunguaji wa Zabuni hizo jijini Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa  Idara ya Ugavi ya Wizara ya Nishati, Armon Macachayo wakati wa kikao cha Zabuni hiyo kilichofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam.

Macachayo alisema kuwa baada ya ufunguaji wa Zabuni husika, Zoezi linalofuta ni kufanyika kwa tathmini ili kupata Kampuni moja itakayokidhi vigezo vya kukabidhiwa mradi.

Zabuni hiyo ilitangazwa   tarehe 30 Agosti, 2017 ambapo Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, ilialika Taasisi Binafsi na Kampuni zenye uwezo kutoka ndani na nje ya nchi kujitokeza kuomba zabuni husika.

Akitoa taarifa za kutangazwa kwa Zabuni husika mwezi  Agosti, 2017, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alisema kuwa Mkandarasi atakayepewa kazi ya kujenga mradi huo ni yule atakayeridhia kujenga mradi husika kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi na kusema kuwa kukamilika kwa mradi husika kutasaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme nchini.

Inatarajiwa kuwa, baada ya zoezi la tathmini na majadiliano ya mkataba wa ujenzi kukamilika, mwanzoni mwa mwezi Januari mshindi wa zabuni hiyo atakabidhiwa Mradi ili kuweza kuanza kazi ya ujenzi wa mradi mara moja.

Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati pamoja na watendaji kutoka kampuni mbalimbali zilizonunua zabuni ya Mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge wakiwa katika kikao cha ufunguaji wa Zabuni hizo jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga alishukuru kampuni zote zilizojitokeza kununua zabuni husika na kuwakaribisha kuwekeza katika miradi mingine ya uzalishaji Umeme.