Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ilifanya ziara wilayani Nzega Mkoa wa Tabora, Machi 17 mwaka huu na kukagua miradi ya umeme inayotekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Iborogero Wilaya ya Nzega, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Machi 17 mwaka huu, kukagua miradi ya umeme vijijini.

Katika ziara hiyo; Kamati ilikagua miradi ya umeme vijijini katika vijiji vya Idala na Kitangiri vilivyoko wilayani Nzega. Pamoja na ukaguzi katika vijiji hivyo, Kamati pia ilipatiwa taarifa fupi ya utekelezaji wa miradi ya umeme kwa Mkoa mzima wa Tabora.

Taarifa iliyowasilishwa na Shirika la Umeme Tanzania Mkoa wa Tabora kwa Kamati hiyo, ilibainisha mambo kadhaa muhimu katika utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani humo kama yalivyoainishwa hapa chini:

 • Ilielezwa kuwa Mkoa wa Tabora unapata umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutokea Mkoa wa Shinyanga, ambao unashushwa mpaka kufikia msongo wa kilovoti 33/11 na kusambazwa katika vituo vya Kiloleni na Lusu, ambavyo navyo husambazia wateja katika maeneo mbalimbali.
 • Mkoa una jumla ya wateja 50,485 ambao kati ya hao; wateja wa matumizi ya kawaida ni 17,070 na wale wa matumizi ya kati ni 33,384 na wateja wa matumizi makubwa ni 31.
 • Gharama zilizotumika katika mradi wa awamu ya kwanza ya upelekaji umeme vijijini katika Mkoa wa Tabora kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni Dola 12,301,744.08 na ulihusisha Wilaya ya Nzega na Urambo.
 • Mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vya Wilaya ya Nzega ulikamilika Novemba 30, 2012 na kufanikiwa kuwaunganisha wateja 967.
 • Mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vya Wilaya ya Urambo ulikamilika Novemba 30, 2012 na kufanikiwa kuwaunganisha wateja 626.
 • Katika awamu ya pili ya umeme vijijini, Mkandarasi CHOCO-CCC (BJ) JV LTD alianza kazi ya

  Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula akizungumza na wananchi wa kijiji cha Iborogero Wilaya ya Nzega, wakati wa ziara ya Kamati hiyo Machi 17 mwaka huu, kukagua miradi ya umeme vijijini.

  kusambaza umeme katika Wilaya zote za Mkoa wa Tabora Februari 17, 2014 na kumaliza Desemba 31, 2016; ambapo jumla ya shilingi 15,342,577,420 na Dola 24,470,598 zilitumika katika utekelezaji.

 • Mkoa umepata miradi ya REA awamu ya tatu, ambapo vijiji 162 vitafikishiwa huduma ya umeme kwa mzunguko wa kwanza.
 • Katika kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tabora, kuna miradi 43 inayotekelezwa na TANESCO. Miradi hii iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji kulingana na upatikanaji wa vifaa vya ujenzi.

Na Veronica Simba – Nzega