Wananchi katika  kijiji cha Zingibari wilayani Mkinga, mkoa wa  Tanga wametoa pongezi kwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati baada ya kuona kasi kubwa ya utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na  Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema kuwa  tangu kupatikana kwa Uhuru  wa Tanganyika mwaka 1961 hawakuwa na ndoto za kupata umeme katika kijiji hicho lakini kuanzia mwaka huu wameanza kuona miundombinu ya  umeme  ikiwekwa  chini ya usimamizi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Seleman Omari, Mwenyekiti wa kitongoji wa Mbuluni alimpongeza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa miradi hiyo ya umeme vijijini na kuongeza kuwa  tangu ameanza kufuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme  vijijini wameshuhudia  kasi ya uwekwaji wa miundombinu ya umeme hususan nguzo.

Alisema katika juhudi za kuunga mkono Wizara ya Nishati katika kuwaunganisha na huduma ya umeme, wameanza kuweka mifumo ya umeme kwenye nyumba zao (wiring) ili kuanza kufaidi huduma hiyo inayotarajiwa kuanza kupatikana hivi karibuni mara baada ya uwekaji wa transfoma katika kijiji husika.

Naye, Mohamed Mengwena mkazi wa kijiji hicho aliongeza kuwa kama vijana wanaamini mara baada ya kuanza kupata huduma ya umeme, wataweza kuboresha shughuli zao za uvuvi kwa kuhifadhi samaki kwenye majokofu na kuuza katika mikoa ya jirani.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza katika mkutano wa hadhara na wakazi hao aliwataka kujiandaa kwa shughuli za kiuchumi, badala ya kutumia umeme kwa matumizi ya majumbani tu.

Katika hatua nyigine aliutaka Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kuhakikisha Taasisi, Shule, Nyumba za ibada, Vituo vya Afya wanapata umeme.

Na Greyson Mwase, Tanga