Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

KAULI YA WAZIRI WA NISHATI KWA...

KAULI YA WAZIRI WA NISHATI KWA BUNGE KUHUSU KUPANDA KWA BEI ZA MAFUTA NA HATUA ZINAZOCHUKULIWA KUSHUGHULIKIA SUALA HILO

Mheshimiwa Spika, tarehe 05 Mei 2022, katika kikao cha kumi na sita (16) cha Mkutano wa Saba (7) wa Bunge la 12, Waheshimiwa Wabunge walijadili kuhusu ongezeko la bei ya mafuta nchini na kutoa maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali. Baada ya mjadala, Mheshimiwa Spika ulitoa maelekezo kwamba, kwa mujibu wa Kanuni ya 56 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Serikali itoe kauli rasmi Bungeni kuhusu hatua za kupunguza athari za kupanda kwa bei za mafuta nchini.

Mheshimiwa Spika, Kabla ya kuendelea, napenda kuwajulisha kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alituita na kutuketisha kitako sisi Wasaidizi wake tukiongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Rais alizungumza mengi, kwa uchungu mkubwa sana. Ameguswa sana na malalamiko na masononeko ya wananchi juu ya kupanda kwa gharama za mafuta na gharama za bidhaa na maisha kwa ujumla. Akasema, hata kama bei iko juu duniani, hata kama takwimu na namba zinaleta mantiki, lakini tutatungulize utu na huruma kwanza katika kulishughulikia suala hili. Bila shaka kwa wale waliomtizama katika Televisheni akiongea na Taifa jana usiku mtakuwa mmeona utu, imani na kujali kwake kulikojaa katika uso wake na katika sauti yake. Isingelikuwa uungwana wake wa kuheshimu mamlaka na mipaka ya Bunge, kauli hii ninayoitoa leo angeitoa yeye muda ule jana. Lakini akaniambia, maadam Bunge lilikuelekeza wewe uwasilishe taarifa, basi busara ya kiuongozi inataka Bunge lisikie taarifa hii kutoka kwako. Hivyo amenituma kuja kwenu leo kuwaletea habari njema.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaufikisha ujumbe huo na kueleza hatua ambazo Serikali inachukua kwenye suala hili, ili kuongeza uelewa na kujenga muktadha, ni vyema nikaeleza mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia na kutoa mnyambulisho wa gharama zinazojumuishwa katika kukokotoa bei za mafuta.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu haina visima vya mafuta wala mitambo ya kuchakata mafuta ghafi. Kama zilivyo nchi nyingi, sisi ni wapokeaji wa bei. Kwa maana hiyo, ni wahanga wa bei za mafuta duniani. Kwa mfano, kwa mafuta ya dizeli, mchango wa bei katika soko la dunia kwenye bei ya mwisho ya mlaji ulikuwa ni asilimia 64 mwezi huu. Na bei za mafuta katika soko la dunia zinatokana na uzalishaji au upatikanaji wa mafuta ghafi (crude oil), upatikanaji wa mafuta yaliyochakatwa (refined petroleum products) na mahitaji ya mafuta (demand of petroleum products).

Mheshimiwa Spika, kwa kiwango kikubwa, uzalishaji na matumizi ya mafuta hutegemea matukio ya kiuchumi na kisiasa hasa katika mataifa yanayozalisha mafuta na yenye uchumi mkubwa duniani. Mfano wa aina ya matukio haya ni kama vile vizuizi vya mauzo ya mafuta vilivyowekwa na nchi za Kiarabu mwaka 1973 (Arab Oil Embargo), Mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979, vita kati ya Iraq na Iran ya mwaka 1980, vita kati ya Iraq na Kuwait mwaka 1990, mdororo wa kiuchumi duniani wa mwaka 2008-2009, na vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa kwenye nchi za Kiarabu (Arab Spring) 2010-13. Matukio haya yaliathiri uzalishaji wa mafuta na kusababisha mahitaji ya mafuta kuwa makubwa kuliko uzalishaji na hivyo kusababisha bei za mafuta kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, Kwa mfano, wakati huo wa vuguvugu la Arab Spring, bei ya mafuta duniani ilifikia dola 126 kwa pipa mwaka 2012 hivyo kupelekea bei ya petroli ya mwezi Aprili 2012 kufikia Shilingi 2,231 kwa lita ambayo ni sawa na Shilingi 3,121 kwa thamani ya Shilingi ya sasa. Bei hii ni sawa na bei ya petroli ya sasa.

Mheshimiwa Spika, vilevile bei ya mafuta duniani ni nyenzo na silaha ya kiuchumi ya nchi zinazozalisha mafuta ambazo zimeunda umoja wao unaoitwa OPEC. Nchi hizi kuna nyakati, kwa makusudi kabisa, hupunguza uzalishaji wa mafuta chini ya uwezo walionao wa kuzalisha ili bei za mafuta ghafi wanayouza zisishuke sana na kuathiri mapato yao.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2020 palitokea mlipuko ugonjwa wa korona ambapo nchi nyingi zilisitisha shughuli za kiuchumi na kijamii (lockdowns) na hivyo kupunguza matumizi ya mafuta. Kutokana na kupungua kwa mahitaji ya mafuta, uzalishaji nao ukasimama. Shida ya kusimama kwa uzalishaji haikuonekana sana kwasababu shughuli za uchumi duniani nazo zilisimama. Katikati ya mwaka 2021, dunia ilipopata chanjo na kuanza kufunguka, kasi ya uzalishaji wa mafuta haikuendana na kasi ya kufunguka kwa uchumi wa dunia.Kukawa na uhaba mkubwa wa mafuta na tukaanza kuona ongezeko la bei ya mafuta hata hapa nyumbani.

Mheshimiwa Spika, wakati huo huo wa Korona, nchi za Urusi na Saudi Arabia, wazalishaji namba mbili na namba tatu wa mafuta duniani duniani, baada ya ugomvi, zilifikia makubaliano ya kupunguza uzalishaji wa mafuta. Kutokana na makubaliano hayo, yaliyozihusisha pia nchi za OPEC, na baadaye kutokana na dunia kufunguka baada ya Korona kuanza kufifia, bei za mafuta hata hapa nyumbani zilipanda kwa kasi. Kwa mfano, bei ya lita ya petroli, ilipanda kutoka shilingi 1,520 mwezi Juni 2020 hadi shilingi 2,511 mwezi Septemba 2021 – ongezeko la zaidi ya shilingi 1,000 katika kipindi kifupi.

Mheshimiwa Spika, ili kupunguza makali ya ongezeko la bei za mafuta nchini, mwezi Oktoba 2021 Serikali ilichukua hatua ya kupunguza tozo zifuatazo:

(a)Tozo ya matumizi ya miundombinu ya bandari (wharfage) inayolipwa kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania;

(b)Tozo ya kuchakata nyaraka za forodha (customs processing fee) inayolipwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA);

(c)Tozo ya kupima na kuthibitisha kiwango cha mafuta kinachopokelewa nchini inayolipwa kwa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA fee);

(d)Tozo ya kupima na kuthibitisha ubora wa mafuta yanayopokelewa inayolipwa kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS charge);

(e)Tozo ya Uwakala wa Meli inayolipwa kwa Shirika la Wakala wa Meli (TASAC fee);

(f)Tozo kwa ajili ya shughuli za udhibiti wa biashara ya mafuta (regulatory levy) inayolipwa EWURA;

Mheshimiwa Spika, zaidi ya tozo hizo, Serikali iliondoa tozo ya huduma (service levy) ambayo wafanyabiashara wa jumla walikuwa wanalipa kwa Halmashauri au Manispaa za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Hii ni

mikoa yenye bandari za kupokelea mafuta na maghala ya kupokea mafuta ya wafanyabiashara hao. Vilevile, Serikali ilipunguza gharama ya kuweka vinasaba kwenye mafuta.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua hizi, tozo zilipunguzwa kwa jumla ya Shilingi 29.38 kwa lita ya petroli; Shilingi 30.05 kwa lita ya dizeli na Shilingi 26.99 kwa lita kwa mafuta ya taa. Kwa hatua hii ya kupunguza tozo, Serikali haitakusanya takribani Shilingi bilioni 102 kwa mwaka na hivyo kutoa unafuu wa bei kwa Wananchi.

Mheshimiwa Spika, wakati tukiwa na mategemeo ya manufaa ya hatua hizo za mwezi Oktoba 2021, miezi miwili baadaye palitokea hofu ya vita kati ya nchi za Urusi na Ukraine. Hofu hii ya vita ilifanya wafanyabiashara wa mafuta duniani kuamini kuwa kungetokea uhaba wa mafuta kwa kuwa Urusi ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa mafuta duniani. Matokeo yake mahitaji ya mafuta katika soko yaliongezeka kuzidi uzalishaji. Vita ilipoanza tarehe 24 Februari 2022, bei za mafuta ghafi ziliongezeka zaidi na kufikia kiwango cha zaidi ya dola za Marekani 100 kwa pipa.

Mheshimiwa Spika, kutokana na vita hii, nchi za Ulaya ziliweka vikwazo vya kiuchumi na vizuizi vya manunuzi ya nishati kutoka Urusi. Kwa vikwazo hivyo, nchi za Ulaya zilianza kununua mafuta kutoka katika nchi za Uarabuni, ambayo sisi ndio tumekuwa tunayategemea na hivyo kuongeza changamoto ya mafuta yaliyopo sokoni kutotosheleza mahitaji. Hali hii ilisababisha bei kuendelea kuongezeka na kufikia tarehe 7 Machi 2022, bei ya mafuta ghafi katika soko la Uarabuni ilifikia dola za Marekani 139 kwa pipa. Bei hii haikuwahi kufikiwa kwa kipindi cha miaka 14 iliyopita. Ifahamike kwamba, kutokana na mfumo wa uzalishaji, uchakataji na usafirishaji wa mafuta, bei ya mafuta yanayoingizwa hapa nchini huakisi bei ya mafuta ghafi kwenye soko la dunia miezi miwili iliyopita. Kwahiyo, bei kubwa tunayoiona leo mwezi Mei hapa nchini kwa sehemu kubwa ni kwamba bei ya mafuta ya mwezi Machi mwaka huu ni kubwa kuwahi kuonekana katika kipindi cha miaka 14 iliyopita.

Mheshimiwa Spika, ukiacha ongezeko la bei za mafuta kwenye soko la mafuta duniani, gharama za kukodi meli za kusafirisha mafuta nazo zimeongezeka. Hii ni kutokana na kwamba bei ya mafuta yanayotumika kwenye meli hizo zimeongezeka na thamani ya mafuta inayobebwa na meli hizo imeongezeka hivyo kuongeza bima, ambayo ni sehemu kubwa ya bei za mafuta. Bima pia imeongezeka zaidi kutokana na hatari ya athari ya vita (war risk premium). Pia, kumekuwepo na uhaba wa meli kutokana na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na nchi za Ulaya kwa Urusi. Lakini pia meli zilizokuwa zinategemewa kutuletea mafuta kutoka Arabuni sasa zinafanya safari za masafa marefu zaidi kwenda Ulaya na hivyo kupunguza upatikanaji wake kwa soko la kwetu. Vilevile, meli nyingi za Urusi zimeondoka kwenye biashara hata ya mafuta yasiyokuwa ya Urusi kutokana na vikwazo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ongezeko la bei za mafuta katika soko la dunia na ongezeko la gharama za uagizaji wa mafuta, bei za mafuta hapa nchini ziliongezeka kwa kiwango kikubwa mwezi Mei 2022 na kufikia Shilingi 3,148 kwa lita ya petroli, Shilingi 3,258 kwa lita ya dizeli na Shilingi 3,112 kwa lita ya mafuta ya taa.

Mheshimiwa Spika, bei hii inajumuisha gharama zifuatazo:

  1. Kwanza, kuna gharama za mafuta ambayo ni bei ya mafuta katika soko la dunia na gharama ya uagizaji wa mafuta hayo inayojumuisha gharama za usafirishaji, bima na faida ya mletaji wa mafuta (supplier). Katika bei za Mei 2022 gharama hizi zilikuwa ni kama ifuatavyo:

(i)Petroli – bei ya soko la dunia ilikuwa ni Shilingi 1,821 kwa lita na gharama ya uagizaji ilikuwa Shilingi 89 kwa lita na hivyo gharama ya mafuta hayo hadi yanafika katika bandari ya Dar es Salaam ilikuwa ni Shilingi 1,910 kwa lita;

(ii)Dizeli – bei ya soko la dunia ilikuwa ni Shilingi 2,088 kwa lita na gharama ya uagizaji ilikuwa Shilingi 54 kwa lita na hivyo gharama ya mafuta hayo hadi yanafika katika bandari ya Dar es Salaam ilikuwa ni Shilingi 2,142 kwa lita;

(iii)Mafuta ya taa – bei ya soko la dunia ilikuwa ni Shilingi 1,917 kwa lita na gharama ya uagizaji

zilikuwa Shilingi 135 kwa lita na hivyo gharama ya mafuta hayo hadi yanafika katika bandari ya Dar es Salaam ilikuwa ni Shilingi 2,052 kwa lita.

Kwa maana hiyo, bei inayotumika kushinda zabuni za kuleta mafuta nchini (premium), ambayo imezungumzwa sana, kwa kawaida inachangia kati ya asilimia 2 na 7 tu ya bei ya mafuta kwenye vituo vya mafuta nchini huku sehemu kubwa ikiwa ni gharama ya bei halisi ya mafuta yenyewe kwenye soko la dunia.

  1. Pili, kuna tozo za Taasisi za Serikali ambazo ni takribani Shilingi 38 kwa lita ikiwa inajumuisha:

(i)Gharama ya matumizi ya bandari inayolipwa TPA ya Shilingi 15 kwa lita;

(ii)Tozo ya huduma (service levy) inayolipwa kwenye halmashauri Shilingi 8 kwa lita;

(iii)Tozo ya Udhibiti inayolipwa EWURA ya kati ya Shilingi 3.20 na Shilingi 5.50 kwa lita;

(iv)Tozo katika biashara ya jumla na rejareja kwa ukaguzi wa miundombinu inayolipwa kwa Wakala wa Vipimo (WMA), Baraza la Mazingira (NEMC), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na Kikosi cha Zimamoto (FRF) ya Shilingi 6.47 kwa lita; na

(v)Tozo ya huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Vipimo (WMA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) wakati ya kupokea mafuta ikiwa ni Shilingi 2.81 kwa lita ya petroli, Shilingi 1.02 kwa lita ya dizeli na Shilingi 4.67 ya lita ya mafuta ya taa.

  1. Tatu, ni kodi za Serikali za Shilingi 920.65 kwa lita ya petroli, Shilingi 800.13 kwa lita ya dizeli na Shilingi 745.77 kwa lita ya mafuta ya taa ambayo inajumuisha:

(i)Tozo ya mafuta ya Shilingi 413 kwa lita ambayo inagawanywa kama ifuatavyo:

a)Shilingi 186 kwa miradi ya TANROADS;

b)Shilingi 177 kwa miradi ya TARURA;

c)Shilingi 50 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji;

(ii)Ada ya mafuta ya Shilingi 100 kwa lita ya petroli na dizeli na Shilingi 250 kwa lita ya mafuta ya taa kwa ajili ya miradi ya kusambaza umeme vijijini;

(iii)Ushuru wa forodha wa Shilingi 379 kwa lita ya petroli, Shilingi 255 kwa lita ya dizeli na Shilingi 465 kwa lita ya mafuta ya taa; na

(iv)Tozo ya maendeleo ya reli ya asilimia 1.5 ya gharama ya mafuta yaliyofikishwa Tanzania. Gharama hii hubadilika kila mwezi kulingana na gharama ya mafuta yanapofikishwa Tanzania. Kwa mwezi Mei 2022, tozo hiyo ni Shilingi 28.65 kwa lita ya petroli, Shilingi 32.13 kwa lita ya dizeli na Shilingi 30.77 kwa lita ya mafuta ya taa.

  1. Nne, ni gharama za uendeshaji wa biashara ya jumla na faida ya wafanyabiashara ambayo kwa ujumla ni Shilingi 161.18 kwa lita ya petroli, Shilingi 160.67 kwa lita ya dizeli na Shilingi 159.36 kwa lita ya mafuta ya taa.
  2. Tano, ni gharama za uendeshaji wa biashara ya rejareja, yaani vituo vya mafuta na faida ya wafanyabiashara hao ambayo kwa ujumla ni Shilingi 118 kwa lita.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, kwa bei za mwezi Mei 2022, tukichukulia dizeli kama mfano, mchango wa kila gharama kwenye bei ya mwisho kwa mlaji ni kama ifuatavyo:

  1. Bei katika soko la dunia – asilimia 63
  2. Gharama ya uagizaji (premium) – asilimia 2
  3. Tozo za taasisi – asilimia 1
  4. Miradi ya barabara na maji – asilimia 13
  5. Ushuru wa Forodha – asilimia 8
  6. Miradi ya REA – asilimia 3
  7. Kodi ya Maendeleo ya Reli – asilimia 1
  8. Gharama za uendeshaji kwa wafanyabiashara wa jumla – 5%
  9. Gharama za uendeshaji kwa wafanyabiashara rejareja – 4%

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa bei ya mafuta ghafi inaendelea kuwa juu, bei ya dizeli inaongezeka kwa kasi zaidi kutokana na uhaba wa mafuta hayo baada ya baadhi ya viwanda vya kusafisha mafuta ghafi (refineries) ya dizeli vilivyopo Afrika, ikiwemo Ghana na Afrika Kusini, kufungwa au kutegemewa kufungwa kutokana na viwango vya sulphur katika mafuta ya dizeli kupunguzwa kutoka 50 kuwa 10 wakati viwanda hivyo havina uwezo wa kuzalisha dizeli yenye viwango vipya. Hivyo, Afrika ya Kusini itaongeza uagizaji wa mafuta yaliyosafishwa kutoka nchi za Uarabuni. Kwa hali hii, ambapo tunagombea soko la dizeli na nchi nyingi zaidi kuliko huko nyuma, bei za mafuta ya dizeli zinategemewa kuongezeka zaidi miezi inayokuja.

Mheshimiwa Spika, katika mjadala wa bei za mafuta kumekuwepo na kulinganisha bei za nchi yetu na bei za nchi za majirani zetu. Kulinganisha bei lazima kuendane na kulinganisha kila kitu – kwa kiingereza wanasema “all things being equal”, ikiwemo viwango vya kodi na tozo

mbalimbali, gharama za kuendesha biashara za mafuta, kama bei zinazowekwa mitandaoni zimejumuisha ruzuku au la, kama tarehe ya kutangazwa bei hizo ilikuwa ni moja, kama ulinganisho huo umetoka kwenye vyanzo rasmi na vya kuaminika, pamoja mambo mengine mengi. Sisi tumeweka kodi ya shilingi 900 kwenye kila lita ya petroli ili tujenge barabara hadi vijijini, tupeleke umeme vijijini, tupeleke maji vijijini, tujenge reli, tukarabati barabara zetu za kitaifa, na tusomeshe watoto bila kulipia karo. Kupanga ni kuchagua. Pamoja na kwamba bado, kila kitu kikipimwa sawa, all things being equal, bado bei zetu ni nzuri kuliko nchi nyingi lakini tukilinganisha bei, tuzingatie kwamba tuliamua kufanya kodi katika mafuta kama chanzo muhimu cha kusukuma maendeleo hasa ya vijijini.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, Oktoba 2021, Serikali ilipunguza tozo za Taasisi za Serikali na hivi sasa tozo hizo zimebaki kuwa ni Shilingi 38 kwa lita. Punguzo zaidi la tozo hizi haliwezi kuleta ahueni kwenye bei ya mafuta kama inavyotegemewa kutokana na kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta kwa kasi. Hata hivyo tutaendelea kuzifuatilia na kufanya uchambuzi wa uhitaji wake. Hivyo basi, kwa kuzingatia kwamba kuondoa tozo za taasisi hakuwezi kutoa nafuu inayotosheleza, na kwa kuzingatia kwamba kodi kubwa kwenye mafuta tunazihitaji kwa maendeleo yetu, Serikali ilianza taratibu za kuchukua mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya kuweka ahueni kwenye bei za mafuta na bidhaanyinginezo zinazogusa maisha ya Watanzania. Mchakato wa kuchukua mkopo huo uko mbioni kukamilika na ahueni kwenye kupanda kwa bei za bidhaa itapatikana katika mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutokana na mahitaji ya wananchi, maoni na ushauri wa Wabunge, maelekezo ya Chama cha Mapinduzi, na ujasiri wa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais alitoa maelekezo kwamba mwaka ujao wa fedha ni mbali. Ahueni itafutwe mapema zaidi. Hivyo basi, kama hatua ya dharura, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwamba, katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha, Serikali ijibane na ijinyime na zitolewe shilingi bilioni mia moja (Shilingi 100,000,000,000) kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini. Ruzuku hii inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2021/22. Kutolewa kwa ruzuku hii hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea. Nafuu nyingine, inayotokana na mikopo niliyoieleza hapa awali, itakuja katika mwaka ujao wa fedha itaelezwa kwa kina zaidi na Waziri wa Fedha kwenye Bajeti ya Serikali mwezi ujao.

Mheshimiwa Spika, ruzuku hii ya shilingi bilioni 100 itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei kuanzia tarehe 1 Juni 2022. Hii ni kutokana na kuwa, wafanyabiashara wa jumla wamekwisha lipia gharama ya mafuta ambayo imejumuishwa katika bei hizi za Mei 2022 na wafanyabiashara wa mafuta katika vituo wamekwishanunua mafuta kwa bei hii inayotumika sasa.

Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zisizo za kifedha zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na:

(i)Kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu kufanya hivyo. Wizara imekamilisha kufanya tathmini ya kampuni zote zilizoonesha nia ya kuweza kuleta mafuta kwa bei nafuu kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wao wa kuleta mafuta hayo ili kuhakikisha uwepo wa mafuta nchini (security of supply). Mipango hii ikileta matokeo yanayotarajiwa, bei za mafuta zitapungua zaidi kuanzia mwezi Agosti 2022.

(ii)Kuanzisha Mfuko wa Kuhimili Ukali wa Bei za mafuta (Fuel Price Stabilization Fund). Serikali imeandaa utaratibu wa kuanzisha mfuko maalumu utakaotumika kupunguza makali ya bei ya mafuta kipindi ambacho bei hizo zinaongezeka kwa kiasi kikubwa. Mpango wa kuanzisha mfuko huu uko katika hatua za mwisho.

(iii) Kuanzisha Hifadhi ya Mafuta ya Kimkakati (National Strategic Petroleum Reserve). Serikali inakamilisha marekebisho ya Kanuni za kuanzisha na kuendesha hifadhi mafuta ya kimkakati ili nchi yetu ijihakikishie usalama wa upatikanaji wa mafuta na unafuu wa bei katika vipindi kama hivi.

(iv) Kuwa na kituokikubwa cha mafuta (Petroleum Hub). Serikali inakamilisha makubaliano ya kujenga maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta kwa ajili ya kuuzwa ndani na nje ya nchi kulingana na uhitaji. Uwepo wa kituo hiki utawezesha nchi kupata mafuta yenye bei nafuu pale bei zinapopanda kupita kiasi.

Mpango huu na utekelezaji wake unaweza kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu.

(v)Kuanzisha upokeaji wa mafuta katika ghala moja (Single Receiving Terminal – SRT) kupitia maghala ya TIPER ili kupunguza au kuondoa gharama za meli kusubiri au kuchukua muda mrefu katika upakuaji wa mafuta katika maghala mengi. Gharama hizi nazo zina mchango katika bei ya mafuta (demurrage charges). Hatua hii itaondoa changamoto za udanganyifu na kuongeza ufanisi katika biashara ya mafuta hapa nchini. Hatua hii inaendana na kuyafanya maghala haya kuwa Customs Bonded Warehouse ili kushamirisha biashara ya mafuta yanayokuja nchini na kwenda kwenye nchi nyingine.

(vi)Kuiongezea uwezo TPDC kuagiza mafuta nje ya nchi, ambapo kwa mara ya mwisho ilifanya shughuli hiyo miaka 20 iliyopita.

(vii)Kuimarisha utendaji na weledi wa taasisi za Serikali zinazoshughulika na biashara ya mafuta nchini, ikiwemo EWURA na PBPA (Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja).

Mheshimiwa Spika, hatua hizi zitafafanuliwa kwa kirefu na fursa ya Wabunge kutoa maoni na ushauri wao wakati wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati wiki tatu zijazo.

Mheshimiwa Spika, bunge lako litakuwa limebaini changamoto za foleni na vurugu katika vituo vya mafuta zilizopo katika nchi nyingine zinazotokana na uhaba wa mafuta. Pamoja na changamoto ya bei, ambalo sio suala letu peke yetu, usimamizi wa sekta ya mafuta hapa nchini, hasa katika kipindi hiki kigumu, umekuwa wa utulivu na wa umakini. Hii sio kwasababu ya ajali bali ni kwa jitihada za makusudi za Serikali kwa ushirikiano na sekta binafsi. Bei za mafuta kupanda ni janga lakini hatari kubwa zaidi hata kwa usalama wa nchi ni kukosekana kwa mafuta. Hili halijatokea hapa kwetu na hatutaruhusu litokee. Leo tunapozungumza tunayo petroli ya kutosheleza kwa mahitaji ya siku 34, dizeli ipo ya kutosheleza kwa mahitaji ya siku 27, mafuta ya taa kwa siku 81 na mafuta ya ndege kwa siku 26. Kanuni zinatutaka tuwe na mafuta ya kutosheleza siku 15 tu. Lakini sisi tunayo ya ziada. Zipo nchi zina shehena ya kutosheleza siku 6 tu. Haya ni mafanikio kwani sote tunafahamu kwamba zipo nchi pia zimelazimika kutaifisha mafuta ya nchi nyingine yanayopitia kwao kutokana na uhaba.

Mheshimiwa Spika, Serikali inawapongeza wadau wa mafuta nchini, hasa kupitia vyama vyao vya TAOMAC na TAPSOA, kwa uelewa wao, ushirikiano wao na uvumilivu wao katika kipindi hiki. Serikali pia inaishukuru Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa ushauri mzuri ambao imekuwa inautoa kwa Wizara katika usimamizi wa sekta. Nakushukuru wewe pia Mheshimiwa Spika kwanza kwa mashauriano na uongozi wako kwenye usimamizi wa sekta lakini pia kwa kutoa fursa kwa Bunge kuchukua nafasi yake kwenye kuisimamia na kuishauri Serikali kwenye suala hili.

Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake na ujasiri wake wa kuchukua hatua ambayo tumeilezea hapa leo. Ni dhahiri kabisa kwamba, yeye binafsi na Serikali yake na Chama anachokiongoza, wanawajali wananchi na wanatoa majawabu kwa mahitaji yao. Binafsi namshukuru kwa kunipa miongozo na kunitia moyo na kunihimiza uvumilivu. Nami namuahidi na kuwaahidi Watanzania kwamba tutaendelea kuisimamia sekta hii kwa uadilifu na weledi. Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa kunipa maelekezo mbalimbali. Namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa usimamizi na maelekezo yake. Namshukuru Mheshimiwa George Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ushauri na maoni mbalimbali na ushiriki wake kwenye suala hili. Namshukuru sana ndugu yangu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, kwa ushirikiano wa karibu wake wakati wote katika suala hili. Na mwisho, lakini sio mwisho kwa umuhimu, nawashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kusimama kidete kuwatetea wananchi wanaowawakilisha na kwa dhamira yao ya kuona sekta inaendeshwa vizuri na nafuu ya bei inapatikana kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

January Y. Makamba (Mb.),

WAZIRI WA NISHATI

10 Mei 2022