Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​MAKABIDHIANO YA DATA ZA UTAFU...

​MAKABIDHIANO YA DATA ZA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI ASILIA KWA VITALU VYA ZANZIBAR

MAKABIDHIANO YA DATA ZA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI ASILIA KWA VITALU VYA ZANZIBAR

Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, tarehe 10/8/2022 ameshuhudia makabidhiano ya data za utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa vitalu vya Zanzibar.

Makabidhiano haya yamefanyika kati ya Waziri wa Nishati wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. January Makamba na Waziri ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame.

Data hizo ni za utafutaji wa mafuta na gesi asilia zilikusanywa kuanzia miaka ya 1950 kutoka katika Vitalu namba 9, 10, 11 na 12 pamoja na Kitalu cha Zanzibar-Pemba, ambavyo vyote vipo Zanzibar.

Kuanzia miaka hiyo ya 1950, kazi ya ukusanyaji wa Data hizo ilifanyika kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ambapo baada ya kutungwa kwa Sheria ya Petroli ya Mwaka 2015 ya Tanzania, kazi hiyo ilihamishiwa kwa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli Tanzania (PURA). Data hizi huhifadhiwa katika mfumo wa kielektroniki (soft copy), nakala ngumu (hard copy), sampuli za miamba (cores) na sampuli za kikemikali (gaseous and liquid).

Data za utafutaji wa mafuta na gesi asilia hukusanywa ikiwa ni moja ya hatua muhimu kuelekea kufanya maamuzi ya maeneo ambayo uchimbaji wa visima utafanyika. Wataalamu huzitafsiri na hivyo kuelewa kama eneo husika lina viashiria vya kuwepo kwa mafuta au gesi asilia.

Katika hafla hiyo PURA na ZPRA wameahidi kuendelea kushirikiana katika maeneo ya Kubadilishana uzoefu katika kuandaa Kanuni, Miongozo na Viwango katika usimamizi wa masuala ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia; Kujenga uwezo katika Ukaguzi wa Mikataba ya Ugawanaji wa Mapato (Production Sharing Agreements – PSA) inayoingiwa baina ya Serikali na wawekezaji katika utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi;

Maeneo mengine ya ushirikiano ni Kuzijengea uwezo taasisi za ZPRA na PURA katika masuala ya usimamizi wa shughuli za Mafuta na Gesi Asilia, kubadilishana wataalamu kwa kupeana uzoefu wa kitaalamu kwa watendaji wa taasisi za ZPRA na PURA; na kubadilishana Data za utafutaji wa mafuta na gesi asilia.