Naibu Katibu Mkuu Nishati aongoza kikao cha Kikundi Kazi cha Taifa cha Nishati Safi ya Kupikia
Naibu Katibu Mkuu Nishati aongoza Kikao kazi cha Kikundi Kazi cha Taifa cha Nishati Safi ya Kupikia
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka ameongoza kikao cha wataalam wa Kikundi Kazi cha Taifa cha Nishati Safi ya Kupikia ili kupitia taarifa mbalimbali zilizoandaliwa na sekretatieti ya kikundi kazi hicho ikiwemo Dira ya taifa ya kuhamia katika matumizi ya nishati safi kupikia na Mpango Mkakati wa utekelezaji wa Dira hiyo.
Kikundi Kazi hicho kimekutana kwa siku tatu kuanzia tarehe 18 hadi 20 Machi, 2023, jijini Dodoma.
Mbuttuka amesema Kikundi kazi hicho kinandaa Dira ya Taifa ya Kuhamia katika Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2033; Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Nishati Safi ya Kupikia 2033; na Muundo wa Mfuko wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuainisha kazi, wajibu, muundo na vyanzo vya fedha.
Kikosi kazi hicho pia kinaandaa rasimu ya katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa kila taasisi inayolisha watu zaidi ya mia tatu (300) ifikapo mwaka 2024 na watu mia moja (100) hadi mia tatu (300) ifikapo mwaka 2025.
Ameongeza kuwa, Kikosi kazi hicho kinapitia na kufanya uchambuzi wa Sera, Mipango na Mikakati mbalimbali iliyopo na kupendekeza maboresho stahiki yatakayohakikisha uwepo wa miongozo yenye utengamano utakaopelekea uendelevu na uwepo wa mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta ya nishati safi ya kupikia.
Kikundi Kazi hicho kinajumuishamaafisa waandamizi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera na Uratibu),Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Wizara ya Kilimo pamoja na Taasisi zinazohusika.
Ikumbukwe kwamba Katika ufunguzi wa Mjadala wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2022, tarehe 1 Novemba 2022, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo mbalimbali katika hotuba yake. Mojawapo ya maelekezo hayo ni kuundwa kwa Kikundi Kazi cha Taifa kitakachojumuisha Serikali, Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo kwa ajili ya kusimamia masuala yote yanayohusika na nishati safi ya kupikia nchini.
Kikundi kazi hicho kiliundwa na kuanza utekelezaji wa majukumu Mwezi Novemba, 2022.