​AfDB yatembelea Mradi wa Umeme wa Zuzu, yaipongeza Wizara ya Nishati


AfDB yatembelea Mradi wa Umeme wa Zuzu, yaipongeza Wizara ya Nishati

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Benki ya Afrika nchini Tanzania, Amos Cheptoo ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwa kusimamia ipasavyo fedha zilizotolewa na benki hiyo kutekeleza miradi ya umeme inayoendelea nchini.

Cheptoo amefanya ziara hiyo Januari 25, 2022 katika Kituo cha Kupoza na Kuzambaza umeme cha Zuzu kilichopo Mkoani Dodoma. Katika ziara hiyo, aliambatana na ujumbe wake pamoja na Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.

Cheptoo alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi ya umeme inayofadhiliwa na Benki hiyo ili kuona utekelezaji wake na hatua iliyofikiwa kutokana na fedha zinazotolewa na Benki hiyo.

Baada ya kuona hali halisi ya utekelezaji wa miradi hiyo, ameeleza kuwa miradi hiyo imefikia hatua nzuri za utekelezaji wake, pia AfDB imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ya Ujenzi, Maji na Nishati.

Awali kabla ya kutembelea miradi hiyo, Mkurugenzi huyo wa AfDB alipata wasaa wa kujitambulisha na kuzungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ambapo pamoja na mambo mengine alimuhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa benki hiyo iko tayari kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo ya aina hiyo kwa lengo la kuiwezesha Tanzania kutimiza azma yake ya kuwapatia wananchi wake nishati ya umeme wa kutosha, na wa bei nafuu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Mramba aliishukuru benki hiyo kwa ushirikiano na mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza sekta ya nishati nchini,na kwamba wataendelea kuitumia Benki hiyo katika ufadhili wa miradi mbalimbali ya nishati inayohitaji fedha katika utekelezaji wake.

Alisema kuwa, Tanzania kama nchi inayoendelea kukua inahitaji zaidi nishati ya umeme katika kuhakikisha kuwa uchumi wake unakuwa na kufikiwa kiwango kitachotakiwa duniani, kwa kuwa na umeme wa uhakika, wakutosha na wa gharama nafuu ili kutimiza malengo iliyojiwekea.

Hata hivyo aliendelea kusema kuwa AfDB, imetoa mchango mkubwa katika miradi ya kuzalisha, kusambaza na kusafirisha umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

Alitaja baadhi ya miradi inayofadhiliwa na AfDB, itakayozalisha umeme kwa kutumia maji pindi itakapokamilika kuwa ni pamoja na Mradi wa Kakonko na Malagarasi.

Aidha mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa msongo wa Kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga, na Tanzania hadi Kenya aliitaja kuwa ni mojawapo ya miradi iliyofadhiliwa na Banki ya AfDB na mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovolti 220 kutoka Rusumo hadi nyakanazi, na Nyakanazi hadi Kigoma wenye msongo wa Kilovolti 400.

Katibu Mkuu Mramba, alisema kuwa licha ya AfDB kufadhili miradi hiyo moja kwa moja, pia kuna baadhi ya miradi mingine imeifadhili kwa kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo ikiwemo Shirika la Maendeleo la Japani (JICA) n.k.