The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

BARAZA LA USHINDANI LATEMBELEA...

BARAZA LA USHINDANI LATEMBELEA WIZARA YA NISHATI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KITAASISI.

Baraza la Ushindani lililo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, leo Mei 18, 2026 limetembelea Wizara ya Nishati iliyopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi katika kusimamia ushindani wa haki pamoja na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kati ya wafanyabiashara na taasisi za umma zinazotoa huduma kwa wananchi.

Ujumbe huo uliongozwa na Bw. Kulwa Msogoti, Mkuu wa Idara ya Uchumi kutoka Baraza la Ushindani, ambaye amesema Baraza la Ushindani lina jukumu la kuhakikisha kunakuwa na ushindani wa haki sokoni kwa kuzuia na kuchunguza vitendo vinavyoweza kuathiri ushindani ikiwemo ukiritimba, ubaguzi wa bei na matumizi mabaya ya nguvu ya soko.

Amesema pia Baraza hilo husimamia utekelezaji wa sheria za ushindani, kushughulikia malalamiko ya wafanyabiashara na watumiaji pamoja na kutoa elimu kwa umma ili kuimarisha uwazi na uwiano katika mazingira ya biashara.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Yusuph Msembele, ameipongeza Baraza la Ushindani kwa hatua hiyo ya kuitembelea Wizara na kueleza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za umma ni msingi muhimu wa kuimarisha utendaji, uwajibikaji na utoaji bora wa huduma kwa wananchi.

Bw. Msembele amesema kuwa Baraza la Ushindani lina mchango mkubwa katika kulinda maslahi ya wananchi na wafanyabiashara kwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira ya soko lenye ushindani wa haki, yanayoepuka ukiritimba, ubaguzi wa bei na matumizi mabaya ya nguvu ya soko, hali inayochochea ufanisi na ukuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya nishati.

Aidha, ameongeza kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana kwa karibu na Baraza hilo katika kubadilishana uzoefu, kuimarisha mifumo ya kiutendaji na kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa rafiki, yenye ushindani wa haki na yanayochochea maendeleo endelevu ya taifa.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wataalamu kutoka idara na vitengo mbalimbali vya Wizara ya Nishati pamoja na wawakilishi kutoka taasisi ya TANESCO, REA na PBPA.