BARAZA LA WAFANYAKAZI WIZARA YA NISHATI LAJENGEWA UELEWA KUHUSU DIRA 2050
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati wamejengewa uelewa kuhusu mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya taifa kuelekea maendeleo ya muda mrefu na endelevu.
Akizungumza Desemba 16, 2025 mkoani Morogoro, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Bw. Titus Kaguo, amesema kuwa kufuatia kukamilika kwa Dira ya 2025, taifa linaelekea katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa Kati Ngazi ya Juu ifikapo mwaka 2050 huku nchi ikiwa na Pato la Taifa la thamani ya dola Trilioni moja.
“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 (Tanzania Development Vision 2025) ilikuwa mpango wa maendeleo wa muda mrefu wa miaka 25 ulioliongoza taifa kuwa na maendeleo endelevu katika nyanja mbalimbali. Utekelezaji wa Dira hiyo umeleta mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali ambapo sekta ya elimu na Afya zimekuwa ni moja ya maeneo zenye mafanikio makubwa. ” Amesema Kaguo
Ametaja vichocheo vya Dira 2050 kuwa ni nishati, usafirishaji fungamanishi, sayansi na teknolojia, utafiti na maendeleo pamoja na mageuzi ya kidijitali
Aidha, wajumbe hao pia walipatiwa elimu kuhusu mafao yanayotolewa na Mfuko wa Pensheni, Akiba na Hifadhi ya Jamii (PSSSF), ambayo ni nguzo muhimu ya ustawi wa watumishi wa umma.
Mafao hayo ni pamoja na pensheni ya uzeeni, mafao ya ulemavu, ajali, uzazi, ugonjwa, mafao ya wafiwa pamoja na msaada wa mazishi. Kupitia mafao hayo, watumishi wa umma na familia zao hupata usalama wa kifedha katika nyakati za dharura na kipindi cha baada ya kustaafu, hatua inayochangia kuboresha maisha na kuimarisha uhakika wa mustakabali wa kifedha.
