The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

BILIONI 275.6 KUIMARISHA UPATI...

BILIONI 275.6 KUIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME MKOANI KAGERA.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange amesema Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa Benaco hadi Kyaka wenye thamani ya shilingi bilioni 275.6 kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika mkoani Kagera pamoja na kuunganisha mkoa huo kwenye Gridi ya Taifa.

Bw. Twange ameyasema hayo Mei 09, 2026 wilayani Ngara mkoani Kagera wakati akiwasilisha taarifa ya mradi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benaco hadi Kyaka pamoja na kituo cha kupoza umeme cha Benaco.

Ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau mbalimbali wa maendeleo ambapo Mfuko wa OPEC unachangia dola za Marekani milioni 60, Mfuko wa Abu Dhabi dola milioni 30, Mfuko wa Saudi dola milioni 13 huku Serikali ya Tanzania ikitoa dola milioni 2.6 kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo.

Aidha, Bw. Twange amefafanua kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Benaco chenye msongo wa kilovoti 220/33 pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benaco wilayani Ngara hadi Kyaka wilayani Missenyi yenye urefu wa takribani kilometa 166.17.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Kagera ambao kwa muda mrefu ulikuwa ukitegemea umeme kutoka nchi jirani ya Uganda.

Sambamba na hilo, amemhakikishia Waziri wa Nishati kuwa TANESCO itaendelea kuwasimamia wakandarasi kwa karibu ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na Mkoa wa Kagera unaunganishwa rasmi kwenye Gridi ya Taifa.