Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

DKT. BITEKO AFANYA MAZUNGUMZO...

DKT. BITEKO AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA BIASHARA WA KOREA KUSINI

Aahidi kuendeleza ushirikiano katika kukuza uchumi

Korea Kusini yaahidi kuwekeza zaidi Tanzania

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Biashara kutoka nchini Korea Kusini, Mhe.Ahn Dukgeun ambapo ameeleza kuwa, Tanzania na Korea Kusini zitaendelea kudumisha ushirikiano uliopo katika nyanja za kiuchumi na kijamii ili kuendelea kuwanufaisha wananchi wa nchi zote mbili.

Katika kikao hicho kilichofanyika Novemba 8, 2023 jijini Dodoma, Dkt. Biteko alimuhakikishia Mhe. Dukgeun ushirikiano kutoka Serikali ya Tanzania katika kukuza uwekezaji na Korea Kusini hapa nchini.

“Niwahakikishie ushirikiano na utayari wa Serikali ya Tanzania katika kuendelea kufungua milango kwa wawekezaji kutoka Korea Kusini muda wowote kwani tayari mahusiano ya nchi zetu mbili yana mizizi iliyokomaa” alisema Dkt. Biteko.

Naye, Waziri Dukgeun amesema kuwa, Korea Kusini itaendelea kuhimiza wawekezaji wengi kuja kuwekeza Tanzania huku akieleza kuwa, moja ya vivutio vikubwa vya uwekezaji Tanzania ni amani na utulivu uliopo ambao unatoa nafasi kwa Wananchi na wawekezaji kuelekeza nguvu na muda wao katika shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi.

“Tutaendelea kuhimiza wawekezaji zaidi kutoka Korea Kusini kuja kuwekeza Tanzania kwani mazingira ya uwekezaji hapa ni mazuri na hali ya utulivu na amani inavutia zaidi kuwekeza bila kuwa na mashaka” alieleza Waziri Dukgeun.

Katika kikao hicho, Waziri wa Biashara kutoka Korea Kusini aliambatana na Balozi wa Korea Kusini hapa nchini Mhe. Kim Sunpyo, Makamu wa Rais wa Benki ya Exim Korea, Ndg. Hon Soon-Young, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Umeme Korea Kusini, Ndg. Shin Myung Jun na Wakurugenzi wengine kutoka Wizara ya Biashara Korea Kusini.