Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

DKT. BITEKO AKAGUA MITAMBO YA...

DKT. BITEKO AKAGUA MITAMBO YA UMEME YA NEW PANGANI (MW 68)

Ataka matengenezo yafanyike kwa kasi na umakini

Aiagiza TANESCO kufanya ukaguzi mara kwa mara kwenye vituo vya umeme

Awasha umeme kijiji cha Ngomeni Muheza

Asifu viongozi wa Tanga kwa umoja walionao

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo amefanya ukaguzi wa mitambo ya umeme inayokarabatiwa katika kituo cha umeme cha New Pangani (MW 68) ambacho kilisimama kuzalisha umeme kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na hitilafu na kuwaagiza Wataalam waTANESCO kufanya kazi hiyo kwa kasi na umakini ili kukamilisha matengenezo hayo ambayo yapo ukingoni.

Katika ziara yake kwenye kituo hicho kilichopowilayani Korogwe mkoani Tanga, Dkt. Biteko aliambatana na viongozi mbalimbali akiwepo Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

“ Nawapongeza kwa hatua mliyofikia sasa kwenye matengenezo, lakini ni muhimu sana kuongeza kasi na umakini katika kumalizia kazi kwani Watanzania wanatutegemea sisi ili kupata umeme wa uhakika.” Amesema Dkt.Biteko

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, matengenezo ya kituo hicho yapo ukingoni na inategemewa kuwa wiki ijayo kitaanza tena kuzalisha umeme na hivyo kuimarisha hali ya upatikanaji umeme hasa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

Aidha ameongeza kuwa, jitihada nyingine zinazofanyika ili kuimarisha hali ya umeme kwenye mikoa hiyo ni kupitia laini ya msongo wa kV 400 itakayotoka Chalinze- Segera hadi Tanga Mjini na laini ya kV 400 kutoka Singida – Manyara- Lemuguru ambayo itaunganishwa na laini ya kutoka Chalinze kwenda Segera hadi Tanga Mjini.

Vilevile, Dkt. Biteko amewataka watendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa, wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vituo vya umeme, jambo litakalowawezesha kutambua mapema endapo kuna hitilafu za umeme na kuzifanyia kazi mapema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Doto Biteko amewasha umeme katika Kijiji cha Ngomeni kata ya Ngomeni wilayani Muheza, Mkoa wa Tanga, na kufanya vijiji vilivyowashiwa umeme wilayani Muheza kufikia 127 kati ya Vijiji 135 sawa na asilimia 95 na katika Vitongoji, Wilaya ya Muheza ina vitongoji 522 na hadi kufikia jana vitongoji 411 vilikuwa vimesambaziwa umeme huku kazi hiyo ikiendelea.

Mara baada ya kuwasha umeme kwenye Kijiji hicho, Dkt. Biteko amesifu umoja uliopo kati ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali katika Mkoa huo, na kueleza kuwa, siri ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ni viongozi kama hao wanaochapa kazi kwa umoja.

Amesema kuwa, viongozi wanapogawanyika wanachelewesha maendeleo na kuwaumiza wananchi kwani wananchi wanachohitaji ni huduma bora kama za umeme na maji, hivyo amewaasa viongozi kupendana na kushirikiana, kwaniwanapimwa kwa matokeo ya maendeleo.

Viongoziwalioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kwa nyakati tofauti wamemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi na kupeleka fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbaliya Maendeleo ambapo mpaka sasa Mkoa wa Tanga umepokea shilingi Trilioni 2.6 kwa ajili ya miradi ya miradi ya Maendeleo.

Fedha iliyotengwa kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini wilayani Muheza ni shilingi Bilioni 18.96 ambayo ni kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye nyumba, migodi midogo, vituo vya afya, maeneo ya kilimo na pampu na za maji huku mkandarasi akiwa ni kampuni ya Derm Group.