Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Dkt. Kalemani apiga marufuku...

​Dkt. Kalemani apiga marufuku upandishaji wa bei ya gesi nchini

Dkt. Kalemani apiga marufuku upandishaji wa bei ya gesi nchini

Hafsa Omar-Dodoma

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewapiga marufuku wauzaji na wasambazaji wa Gesi za majumbani kupandisha bei ya bidhaa hiyo.

Amepiga marufuku hiyo Agosti 18, 2021, Jijini Dodoma alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye maduka mbalimbali kwa wauzaji wa gesi hiyo.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, Serikali haitakubali kuona wafanyabiashara wanajipangia bei kubwa ambazo zinawaumiza Watanzania.

“Ninawapa onyo la mwisho wafanyabiashara wote wa gesi za majumbani kutopandisha bei, pia Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) walishatoa maelekezo, Mimi Waziri wa Nishati napita sasa kutoa onyo la mwisho, tukirejea wakati mwingine na kukuta bei imepanda tutachukua hatua ikiwa ni pamoja na kukufungia biashara husika kwa mtuhumiwa”, alisisitiza Dkt.Kalemani.

Alifafanua kuwa, Mtungi wa ujazo wa kilo 6 unatakiwa kuuzwa kati ya shilingi 20, 000 hadishilingi 21,000 na Mtungi wa ujazo wa kilo 15 unauzwa kati ya shilingi 47,000 hadi shilingi 50,000 na bei hiyo ni kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

Aidha, alisema kuwa Serikali inafahamu bei ya gesi katika soko la dunia imepanda lakini si kwa kiasi kikubwa ambacho inawafanya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa hiyo hata kuliko namna ilivyopanda katika soko la dunia.

“Serikali inaendelea kufuatilia bei ya Soko la dunia na kama bei itapanda sana mtaelekezwa na kupewa utaraibu na EWURA lakini kwasasa haitapanda hatutaki kuleta kero kwa wananchi alisema”, alisema Dkt. Kalemani.

Hata hivyo, aliwataka wafanyabiashara hao endapo watapata changamoto yoyote wawasiliane na EWURA ili waweze kupewa utaratibu unaotakiwa.

Pia, aliwaagiza Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuchukua hatua kali kwa yoyote ambae atakiuka maagizo hayo.