DKT.MPANGO ATAKA AFRIKA KUUNGANISHA NGUVU UENDELEZAJI WA JOTOARDHI
Aeleza umuhimu wa Sekta Binafsi kuhusishwa uendelezaji Jotoardhi
Akaribisha uwekezaji katika vyanzo vya Jotoardhi Tanzania
Kapinga amshukuru Dkt.Samia kwa Dira inayoiimarisha Sekta ya Nishati
Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amesema Bara la Afrika
linapaswa kuunganisha nguvu na kushirikiana ili kuweza kuendeleza
ipasavyo nishati ya Jotoardhi ambayo ni safi na endelevu na kuondokana
na nishati zisizo safi katika kuzalisha umeme ikiwemo mafuta mazito.
Dkt.Mpango amesema hayo jijini Dar es Salaam tarehe 23 Oktoba, 2024
wakati akifungua Kongamano la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) ambalo
limehudhuriwa na washiriki 800 kutoka nchi 21 duniani.
Aidha, amesema kila nchi inapaswa kuwa na Taasisi maalum kwa ajili ya
kusimamia uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi na kuwa na kanuni na
sheria madhubuti zitakazowezesha sekta binafsi kushiriki katika
uendelezaji wa nishati hiyo.
Vilevile ameziasa nchi zenye Nishati ya Jotoardhi kufanya mazungumzo
ya kimkakati na Taasisi za kifedha ikiwemo Mabenki ili kupata fedha za
kuendeleza nishati hiyo kutokana kuhitaji fedha nyingi katika
uendelezaji wake badala ya kutegemea bajeti za Serikali pekee.
Amesema mipango ya Tanzania ni kuwa na umeme wa kiasi cha zaidi ya
megawati 5000 ifikapo mwaka 2030 kutoka vyanzo mchanganyiko huku
nishati jadidifu ikipewa kipaumbele ikiwemo Jotoardhi, upepo na Jua.
Ameeleza kuwa, Tanzania iliamua kwa vitendo kuendeleza nishati ya
Jotoardhi kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuanzisha Taasisi
inayosimamia sekta husika mwaka 2014 ambayo moja ya kazi zake ni
kusimamia uendelezaji wa nishati hiyo.
Amesema tayari Tanzania imekamilisha utafiti wa awali kwenye baadhi ya
maeneo matano yenye viashiria vya Jotoardhi kwenye Bonde la Ufa na
sasa kuna uchorongaji unaoendelea katika eneo la Ngozi ili kuhakiki
uwepo wa nishati hiyo.
Ameongeza kuwa, hatua nyingine iliyopigwa kwenye Jotoardhi nchini ni
kuongezeka kwa idadi ya wataalam waliobobea katika masuala ya nishati
hiyo na ununuzi wa rig itakayotumika kwa ajili ya shughuli za
uchorongaji kwenye maeneo yenye mashapo ya Jotoardhi.
Amewashukuru Wadau mbalimbali wa maendeleo wa wanaoiunga mkono
Tanzania kifedha na kiufundi ili kuendeleza nishati ya Jotoardhi
ikiwemo Japan, Iceland na Ireland.
Katika kongamano hilo, Dkt. Mpango amewakaribisha Wawekezaji ili
kuendeleza nishati ya Jotoardhi katika vyanzo mbalimbali ikiwemo Ngozi
(70MW), Kiejo-Mbaka (60MW), Songwe (kati ya 5 na 35MW), Natron
(60MW) na Ruhoi (5MW).
Pia amekaribisha washiriki wa ARGeo-C10 kufanya uwekezaji kwenye
sekta mbalimbali ikiwemo ya madini na kufanya utalii katika vivutio
mbalimbali ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Ngorongoro n.k
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Capt. George
Mkuchika amesema chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan sekta ya
nishati imezidi kupiga hatua ambapo umeme vijijini umefika kwa
takriban asilimia 98 na ifikapo Desemba mwishoni vijiji vyote vitakuwa
vimesambaziwa.
Ameeleza kuwa hali hiyo ni kielelezo cha mahitaji ya umeme kuongezeka
hivyo lazima uendelezaji wa vyanzo mchanganyiko vya nishati uongezeke
ikiwemo Jotoardhi ambayo ikiendelezwa itaweza kuzalisha umeme wa
megawati 5000.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Mafuta kutoka Kenya, James
Wandayi amesema kuwa nchi hiyo tayari imepata mafanikio katika nishati
ya Jotoardhi kwani kwa sasa zaidi ya asilimia 45 ya umeme nchini humo
unazalishwa na Jotoardhi.
Amesema Nishati ya Jotoardhi inapaswa izidi kupigiwa chapuo barani
Afrika kutokana na kuwa ni endelevu ambapo licha ya kutumika kuzalisha
umeme inatumika pia kwenye sekta nyingine ikiwemo kilimo na ufugaji.
Awali, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alimshukuru Rais,
Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kujitoa kwake katika kuendeleza Sekta ya
Nishati na uongozi wake unaotoa Dira katika kushughulikia masuala
mbalimbali yanayohusu Sekta.
Amesema Jotoardhi itawezesha azma ya Tanzania kuwa na umeme unaotokana
na vyanzo mchanganyiko huku lengo likiwa ni kuzalisha kiasi cha
megawati 995 kutokana na nishati hiyo ifikapo mwaka 2024 hali
itakayoongeza pia usalama wa gridi ya umeme.
Amesema nishati ya Jotoardhi ni suluhisho muhimu katika utatuaji wa
changamoto za upatikanaji wa nishati ya kutosha barani Afrika ambayo
inaenda sambamba na mipango ya dunia katika kupunguza uzalishaji wa
hewa ya ukaa.
Hafla ya ufunguzi wa Kongamano la ARGeo-C10 imehudhuriwa na viongozi
mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge,
Mabalozi wa nchi mbalimbali, Madiwani, Wadau wa Maendeleo na Watendaji kutoka Taasisi za Serikali na Binafsi