The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

DKT. NCHIMBI: WIZARA ZA KISEKT...

DKT. NCHIMBI: WIZARA ZA KISEKTA ZITUMIE FURSA BIASHARA YA KABONI KUKIJANISHA TANZANIA.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi. Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amezihimiza Wizara za kisekta kujumuisha fursa zilizopo katika biashara ya caboni katika mpango yao kuchangia uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu nchini.

Akizungumza leo Juni 05, 2026 katika hafla yaMaadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Dkt. Nchimbi amesema biashara ya caboni ni miongoni mwa nyenzo muhimu zinazowezesha sekta mbalimbali kushiriki kikamilifu katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku zikichochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, amepongeza wadau mbalimbali kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa ajenda ya nishati safi nchini, akieleza kuwa ushiriki wao unaongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira.

Amesema matumizi ya nishati safi yana mchango mkubwa katika kupunguza uharibifu wa mazingira, kuhifadhi misitu na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa unaochangia mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Nchimbi amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wananchi ili kuhakikisha malengo ya uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi yanafikiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani mwaka 2026 yamehitimishwa hii leo yakiwa sambamba na kaulimbiu isemayo: “Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania”.