The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

DRC YAFANYA ZIARA YA MAFUNZO K...

DRC YAFANYA ZIARA YA MAFUNZO KUHUSU USIMAMIZI WA MAFUTA TANZANIA.

Waziri wa Hydrocarbons wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mhe. Acacia Bandubola Mongo, amesema nchi yake itaendelea kujifunza kutoka Tanzania kuhusu usimamizi bora wa sekta ya mafuta ili kuboresha mifumo yake ya upatikanaji na usambazaji wa nishati hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya mafuta ya Kurasini Oil Jet (KOJ-1), iliyopo Bandari ya Dar es Salaam Mei 8, 2026, Mhe. Bandubola ameipongeza Tanzania kwa kusimamia kwa uwazi na ufanisi uagizaji wa mafuta kwa pamoja.

Amesema Congo DRC inategemea kwa kiasi kikubwa miundombinu ya Tanzania katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika, na kuongeza kuwa ziara hiyo imelenga kujifunza kwa vitendo namna mafuta yanavyopokelewa, kuhifadhiwa na kusimamiwa bandarini.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), ambaye ni Meneja Mipango ya Petroli, Bw. Gilbert Jungulu, alieleza kuwa PBPA inasimamia kwa karibu shughuli za upakuaji na upakiaji wa mafuta kupitia mfumo wa kisasa wa SCADA.

Aliongeza kuwa matumizi ya mfumo huo yamewezesha kupunguza kwa kiwango kikubwa upotevu wa mafuta na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mnyororo mzima wa ugavi wa mafuta nchini.