The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

ELIMU YA CNG NA TEKNOLOJIA ZA...

ELIMU YA CNG NA TEKNOLOJIA ZA NISHATI SAFI ZIWAFIKIE WANANCHI WA KIPATO CHA KAWAIDA: MHE. KUNDO.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Kundo Mathew, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha teknolojia za kisasa ikiwemo matumizi ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) kwenye magari, pamoja na mifumo mingine ya nishati safi, zinawafikia wananchi wa kipato cha kawaida ili waweze kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya sekta hiyo.

Mhe. Kundo ameyasema hayo alipotembelea banda la Wizara ya Nishati katika Maonesho ya Wiki ya Mazingira Duniani 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Center.

Akiwa katika banda hilo, alijionea miradi na teknolojia mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara ya Nishati, ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia, mifumo ya nishati jadidifu pamoja na magari yanayotumia nishati mbadala.

Miongoni mwa teknolojia zilizovutia zaidi katika ziara hiyo ni gari linalotumia gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) pamoja na gari la umeme, ambavyo vinatajwa kuwa sehemu ya suluhisho la kupunguza gharama za usafiri na kupunguza athari za mazingira zitokanazo na matumizi ya mafuta ya kawaida.

Akitoa maelezo kwa Naibu Waziri huyo, Afisa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati, Bi. Spora Sulle, amesema maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara pamoja na manufaa ya matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya nishati.

Bi. Sulle ameeleza kuwa wananchi wanaotembelea banda hilo wanapata nafasi ya kujionea kwa vitendo namna magari ya umeme na yale yanayotumia CNG yanavyofanya kazi, sambamba na kupata elimu kuhusu mchango wake katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya uchumi wa taifa.

Maonesho ya Wiki ya Mazingira Duniani 2026 yanaendelea chini ya kauli mbiu isemayo “Dira 2050: Tuwekeze Kukijanisha Tanzania”, yakilenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na uwekezaji endelevu kwa maendeleo ya Taifa.