The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

ELIMU YA LISHE BORA NA NISHATI...

ELIMU YA LISHE BORA NA NISHATI SAFI YA KUPIKIA INAHITAJIKA ZAIDI KWA WANANCHI

Serikali imesema kuwa elimu ya lishe bora na matumizi ya nishati safi inahitajika zaidi kwa wananchi ili wafahamu namna ya kuboresha afya ya familia na kutunza mazingira.

Hayo yameelezwa na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia wa Wizara ya Nishati, Bi. Zuena Msuya wakati wa kuhitimisha maadhimisho ya siku ya lishe na nishati safi ya kupikia katika wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma.

Msuya amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa nishati safi ikiwemo sekta binafsi na washirika wa maendeleo wataendelea kushirikiana katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kuhakikisha watanzania wanapata elimu sahihi ya mapishi, lishe nora na matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya na kutunza mazingira.

Pia kufikia lengo la kufukia asilimia 80 za watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

“ Ni jambo la faraja kuona utekelezaji wa mradi huu kwa wilaya ya Kongwa unaonekana kupitia mradi wa Boresha Mazingira, Tumia Jiko Banifu na lengo ni kusambaza majiko banifu 26,000 ifikapo 2029 na tayari majiko 15,000 yameshasambazwa katika wilaya hiyo."

"Hii ni hatua kubwa inayochangia moja kwa moja kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuimarisha afya za familia zetu kwa kuwa,” alisema Msuya.

Amesema kupitia mafunzo ya vitendo kwa wananchi kuhusu lishe bora na nishati safi kwa kutumia majiko banifu, hugusa familia moja kwa, mafunzo hayo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hulenga moja kwa moja hivyo kuimarisha lishe ili kuboresha afya na mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha na Teknolojia ya Nishati Mbadala kutoka Italia (Offgridsun) Valentina Quaranta amesema lengo la kutekeleza mradi huo ni kuunga mkono Serikali ya Tanzania ya kuwafikia wananchi wote nchini ili kuondokana na matumizi ya nishati isiyo salama, kutunza mazingira na kupunguza hewa ya ukaa duniani.

Kwa Mwaka 2028 wamepanga kusambaza

majiko banifu 300,000 ya itanufaisha wilaya sita nchini ambazo ni Kongwa, Chamwino, Bahi, Handeni na Shinyanga ambazo mradi huo utatekelezwa hatua kwa hatua tofauti ambapo kwa kuanzia sasa watasambaza majiko 200,000 kwa wilaya nne nchini.

Akizungumzia wilaya hizo Quaranta amesema Shirika hilo limepanga kusambaza majiko banifu 52,000 katika Wilaya ya Kongwa, majiko 50,000 Chamwino, Handeni majiko 40,000 na Longido majiko 20,000 ifikapo mwaka 2027.