ELIMU YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YAENDELEA KUTOLEWA KWA WANANCHI
Imeelezwa kuwa Mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia unalenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda afya za wananchi, kupunguza gharama za maisha, na kuimarisha uchumi kwa kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma, elimu na miundombinu muhimu ya kutumia nishati safi ya kupikia.
Hayo yameelezwa Novemba 21, 2025 Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkururugenzi wa Nishati safi ya kupikia Wizara ya Nishati Bw. Ngereja Mgejwa wakati akiongea katika kipindi cha Alasiri Lounge Azam TV.
Akiwa katika kipindi hicho Mgejwa ameeleza kuwa mpango jumuishi wa kupambana na athari za kimazingira, kiuchumi na kijamii umeendelea kupewa kipaumbele nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya Kupikia unaolenga kuboresha afya, mazingira na uchumi wa wananchi.
“Msingi wa mkakati huu unajikita katika kuhakikisha kuwa ifikapo 2034 asilimia 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia kwani hata hivyo muitikio ni mkubwa kutokana na kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja takwimu zinaonesha kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yamefikia asilimia 23% hivyo ni imani yetu kuwa elimu tunazoendelea kuzitoa kwa jamii zitaondoa mitazamo hasi ya wanannchi katika matumizi ya mkaa na kuni ambapo hadi kufikia 2034 asilimia 80% ya Watanzania wataanza kutumia nishati safi ya kupikia”. Ameeleza Bw. Ngereja.
Aidha ameendelea kusema kupitia mkakati huo kumekuwa na ubunifu kwenye sekta ya nishati safi, kwani kutokana na mitungi ya gesi kupewa msamaha wa kodi kampuni kadhaa kuanza kuuza mitungi ya gesi kwa bei nafuu ili kuongeza upatikanaji wake huku akieleza kuwa juhudi zinafanyika kuhakikisha bei za kujaza mitungi zinakuwa chini ili kumrahisishia mwananchi wa kawaida.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi. Neema Mbuja ameeleza kuwa katika utekelezaji wa mkakati wa taifa wa nishati safi ya kupikia Serikali imeanzisha na kuimarisha mkakati mahususi wa mawasiliano unaolenga kuhakikisha taarifa sahihi kuhusu nishati safi ya kupikia zinawafikia wananchi wote kwa wakati.
“Mkakati wa Mawasiliano unahusisha matumizi ya njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo vyombo vya habari, matangazo, kampeni za kijamii, pamoja na ushirikishwaji wa wananchi hususani wanawake, vijana, watoto na taasisi mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha ya matumizi ya nishati pamoja na aina zote za nishati safi ya kupikia ili waweze kuchagua aina bora ya nishati safi ya kupikia kulingana na uhitaji wao”. Ameeleza Bi. Mbuja.
Ameeleza kuwa kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati (TANESCO, TPDC, REA) elimu imeendelea kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali huku wakihakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kirahisi na kwa gharama nafuu.
Kwa ujumla, mpango huu unalenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, kulinda afya za wananchi, kupunguza gharama za maisha, na kuimarisha uchumi kwa kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma elimu na miundombinu muhimu ya kutumia nishati safi ya kupikia.
