Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

EWURA ZINGATIENI MASLAHI YA NC...

EWURA ZINGATIENI MASLAHI YA NCHI KATIKA SHUGHULI ZA UDHIBITI WA MAFUTA NA MAJI - DKT. BITEKO


Awapongeza kwa kushusha gharama za uagizaji mafuta.

Asisitiza EWURA kudhibiti vitendo vya urasimu na rushwa mahali pa kazi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
amewataka Watendaji na Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA) kuzingatia maslahi ya Watanzania na maslahi ya
nchi katika kazi zao za Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ili
Watanzania wapate huduma bora na kwa unafuu mkubwa.

Dkt. Biteko amesema hayo wakati akifungua Kikao cha Baraza la Pili la
Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kilichofanyika tarehe 8 Novemba, 2023
jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Naibu
Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemalira Rutatinwa na Mwakilishi wa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Bi. Ziana Mlawa.

“Tambueni kuwa Taifa lina mategemeno makubwa na ninyi, hivyo fanyeni
kazi zenu kwa weledi na ubunifu mkubwa unaoendana na kasi ya
teknolojia na maendeleo ya dunia; kanuni na miongozo yenu mnayotumia
katika utekelezaji wa majukumu iundwe katika mifumo rafiki kulingana
na hali iliyopo ili ilenge kuleta matokeo chanya kwa ustawi wa Taifa
na hivyo Watanzania waendelee kupata huduma bora na kwa gharama
stahiki.” Amesema Dkt. Biteko

Pia amewataka Watumishi wa EWURA kuweka mkazo kwenye kudhibiti vitendo
vya urasimu na rushwa mahali pa kazi, kutoangalia maslahi binafsi
wakati wa kutenda kazi ili kuepusha kuwaumiza Watanzania walio wengi,
na ametoa wito kwa wafanyakazi hao kumkemea mtu yeyote anayeonekana
kuwa na vitendo vya rushwa na ubinafsi katika eneo la kazi.

Vilevile, amewasisitiza Wafanyakazi wa EWURA kuwajibika ipasavyo
katika kutekeleza majukumu yao kwa kuhakikisha kuwa Watoa Huduma
wanafanya ushindani wenye tija na ufanisi wa kiuchumi, kulinda maslahi
ya Walaji na mitaji ya kifedha ya Watoa Huduma pamoja na kuhakikisha
upatikanaji wa huduma kwa makundi yote ikiwemo ya watu wanaoishi
vijijini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu ameipongeza EWURA kwa kupitia
upya gharama za uagizaji wa mafuta ambazo amesema kuwa, awali zilikuwa
kubwa na zilikuwa zikipelekea athari mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa
gharama katika Sekta ya Usafirishaji na Uzalishaji.

“Gharama hizi za uagizaji mafuta zilikuwa kubwa mno huku kukiwa hakuna
sababu ya kuwa kubwa kwa kiasi hicho, niliwapa maelekezo mkazitazame
upya, nashukuru mmeziangalia na ninafurahi kwamba zimeshuka na hivyo
kupunguza makali kwa watumiaji." Amesema Dkt. Biteko.

Vilevile Naibu Waziri Mkuu ameiagiza TUGHE- Taifa kueleza juhudi
zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuhusu masuala ya
Wafanyakazi akitolea mfano upandishwaji madaraja wa mseleleko kwa
watumishi ambao hawajapanda madaraja kwa muda mrefu. Amewataka pia
kuwashirikisha wanachama wao ili kuisaidia Serikali katika kupeleka
maendeleo kwa wananchi na pia kuikumbusha Serikali kutimiza wajibu
wake kwa Wafanyakazi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile alisema kuwa,
Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi lengo
likiwa ni kuhakikisha Huduma za Nishati na Maji zinapatikana kwa
uhakika, kwa kutosha, kwa uendelevu na kwa gharama ambazo wananchi
wanazidumu.

Alimshukuru, Dkt. Biteko kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Taasisi hiyo
na miongozo anayotoa ambayo inafanya EWURA iendelee kuboresha utendaji
wake katika kuhudumia Watanzania.

Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa EWURA kinachoendelea jijini Dodoma
kimelenga kujadili masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa Bajeti ya
EWURA kwa mwaka 2022/2023 na Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za EWURA za
mwaka 2022/23.