The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

HANNYG INVESTMENT YAONGEZA KAS...

HANNYG INVESTMENT YAONGEZA KASI YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI KUPITIA TEKNOLOJIA YA KUNI POA (BRIQUETTES).

Kampuni ya HannyG Investment imeendelea kuwa kinara katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa Kuni Poa (Briquettes), bidhaa mbadala ya kuni na mkaa inayolenga kulinda mazingira na kuboresha upatikanaji wa nishati nafuu kwa wananchi.

Akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Nishati Safi ya Kupikia unaoendelea jijini Arusha, Mkurugenzi wa HannyG Investment, Bi. Hanny Mbaria amesema kampuni hiyo imejikita katika kuzalisha briquettes zenye ubora wa hali ya juu ambazo hutoa joto la kutosha kwa muda mrefu, hivyo kuwa suluhisho bora kwa kaya na taasisi zinazotegemea kuni na mkaa wa kawaida.

Bi. Mbaria alieleza kuwa matumizi ya Kuni Poa yanachangia kupunguza ukataji miti holela, kuhifadhi mazingira na kupunguza gharama za nishati kwa watumiaji. Aidha, alisema bidhaa hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiendesha kampeni za elimu kwa umma kuhusu faida za briquettes na umuhimu wa kuhamia kwenye vyanzo vya nishati endelevu na rafiki kwa mazingira.

Kwa upande mwingine, HannyG Investment inaendelea kupanua mtandao wake wa usambazaji katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya kutumia nishati hiyo mbadala kwa urahisi na gharama nafuu.