Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA...

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI MRADI WA UMEME MKOANI ARUSHA

Mradi wagharimu takribani Dola milioni 258

Kunufaisha nchi zipatazo 13

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya ziara Mkoani Arusha kukagua mradi wa ujenzi wa njia kuu ya umeme wenye msongo wa kilovoti 400 katika eneo la Lemugur mkoani Arusha tarehe 13 Machi, 2024.

Wakiongozwa na mwenyeji wao Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga wajumbe wa Kamati hiyo walifanikiwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kitakachounganisha Tanzania na nchi za Afrika mashariki pamoja na Kusini mwa Afrika katika ushirikiano kwenye sekta ya nishati ya umeme.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Judith Kapinga aliwashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kwa kufanya ziara na kutoa ushauri na maelekezo muhimu yanayolenga kufanikisha utekezaji wa mradi huo utakaokuwa mkombozi wa upatikanaji wa umeme katika mkoa wa Arusha na nchi zipatazo 13.

Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa kituo hicho takribani dola milioni 258

“Tunamshukuru Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwajili ya Miradi ya Nishati na hasa katika kituo hiki ambacho kitakua fursa ya Biashara ya Nishati ya Umeme kwa upande wa Nchi za kusini na Kaskazini", alisema Mhe. Kapinga

Aidha, Mhe. Kapinga alisema baada ya kukamilika kwa mradi huu tutakuwa na uhakika wa umeme nchini kwa kuwa miundombinu hii itawezesha kusafirisha umeme nje ya nchi na pia kuleta umeme kutoka katika nchi hizo pale tunapokuwa na uhaba wa nishati hiyo.

Mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya dola za Marekani 258.82 utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 99.6 hadi sasa.

Pia, amepokea ushauri na maelekezo yote ya Kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kuanzia na eneo la usimamizi wa miradi ya umeme ili iweze kumaliza changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme hapa nchini.

Akitoa maelekezo ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mathayo David Mathayo amelekeza wizara kuhakikisha inasimamia wakandari wote wanaotekeleza miradi ya umeme nchini ili wakamilishe miradi hiyo kwa wakati na kuiwezesha Serikali kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi wote kama ilivyokusudiwa.

“Kumekuwa na miradi ya umeme ambayo utekelezaji wake unasuasua kutokana na uzembe unaofanywa na baadhi ya wakandarasi wasio waaminifu waliopewa kazi hizo hivyo Wizara ikahakikishe inawachukulia hatua ikiwemo kuwafungia leseni zao ili wasiwe na sifa za kupata kazi katika nchi yetu”. Alisema.

Ziara hiyo imeudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini Tanesco Mha. Gissima Nyamo-Hanga na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Tanesco.