KAMPENI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA; NI WILAYA KWA WILAYA
Elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeendelea kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika vijiwe vya draft, vijiwe vya kahawa, masoko na vituo vya mabasi nchini lengo likiwa ni kuhakikisha watu wanaachana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia kama vile kuni na mkaa.
Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) inaendelea na kampeni endelevu ya nishati safi ya kupikia ambapo tarehe 17 Februari 2026 kampeni hiyo iliwafikia wananchi katika Kata ya Mkata, wilayani Handeni mkoani Tanga.
Timu ya uhamasishaji imekuwa ikizungumza na wananchi na wafanyabiashara ili kubaini nishati wanayotumia na kuwapatia elimu ya umuhimu wa kuhamia katika nishati safi.
Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa wanahitaji kutumia gesi zaidi wanapopika hivyo wameomba Serikali kuweka gharama rafiki za ununuzi wa nishati hiyo.
Katika kampeni hiyo wananchi wanapata fursa ya kuoneshwa namna majiko ya gesi na umeme yanavyopika haraka na kwa gharama nafuu. Pia wamepata fursa ya kuonja chakula kilichoandaliwa kwa teknolojia hizo na kukiri kuwa kina ladha nzuri tofauti na dhana iliyokuwepo awali.