The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

KAMPENI YA NISHATI SAFI YA KUP...

KAMPENI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YAFIKA MASOKONI, VITUO VYA MABASI HANDENI

Kampeni ya nishati safi ya kupikia imeendelea kuwafikia wananchi katika masoko na vituo vya mabasi wilayani Handeni mkoani Tanga ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa wananchi.

Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) inaendesha kampeni hiyo inayolenga kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Katika utekelezaji wake, timu ya uhamasishaji imetembelea masoko na vituo vya mabasi huku ikizungumza na wananchi na wafanyabiaahara ili kubaini aina ya nishati wanayotumia na kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia.

Baadhi ya wafanyabiashara katika Soko la Chogo na Soko Kuu la ndani wameeleza kuwa hutumia gesi wanapokuwa na haraka ya kupika, lakini bado hutegemea nishati nyingine zisizo safi katika matumizi ya kawaida.

Kutokana na hilo, timu ya uhamasishaji imewasisitiza kuendelea nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi na umeme kwa matumizi ya kila siku, ikibainisha kuwa nishati isiyosafi ni hatari kwa afya na mazingira.

Aidha, wananchi wamepatiwa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuoneshwa namna majiko ya gesi na majiko ya umeme yanavyoweza kupika chakula kwa haraka na kwa gharama nafuu,

Kivutio kikubwa katika kampeni hiyo, ilikuwa ni suala la wananchi kupata fursa ya kuonja chakula kilichoandaliwa kwa kutumia teknolojia hizo za umeme na gesi ambapo wamekiri kuwa chakula hiko kina ladha nzuri tofauti na dhana iliyojengea kuwa chakula kinachopikwa kwa nishati safi kinakuwa hakina ladha nzuri kama ukipikia kwa kutumia kuni na mkaa.