KAMPENI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YAZIDI KUSAMBAA MAENEO MBALIMBALI JIJINI DODOMA.
Wafanyabiashara wa soko la Mavunde Chang’ombe, Jijini Dodoma, wamepatiwa elimu kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji hilo.
Kampeni hiyo imelenga kuongeza uelewa kwa jamii na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala iliyo salama kwa afya na rafiki kwa mazingira.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Bw. Deo Alex mtaalamu kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia alieleza kuwa matumizi ya nishati safi yana mchango mkubwa katika kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi wa kuni na mkaa.
Alisisitiza umuhimu wa wananchi na wafanyabiashara kuhamia kwenye teknolojia safi za kupikia ili kulinda afya na mazingira.
Aidha, Bw. Alex alibainisha kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi unakuwa rahisi na wa gharama nafuu, hususan kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kati wanaojihusisha na shughuli za upishi.
Katika kampeni hiyo, timu ya wataalamu ilikutana na mwenyekiti wa soko la Mavunde Chang’ombe Bw. Godfrey Mbilinyi, ambapo mafunzo hayo yaliambatana na onesho la vitendo la matumizi ya Teknolojia za Nishati Safi ya Kupikia.
Hali hiyo iliwasaidia wafanyabiashara kuelewa kwa vitendo namna bora ya kutumia teknolojia hizo katika shughuli zao za kila siku.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Bw. Mbilinyi alisema kuwa elimu hiyo imekuja kwa wakati muafaka, ikisaidia kuboresha mazingira ya kazi ndani ya soko na hata majumbani.
Aliongeza kuwa matumizi ya nishati safi yatapunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuahidi kuendelea kuhamasisha wafanyabiashara wote kutumia teknolojia hiyo.