The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

KITUO CHA EV - CHARGING STATIO...

KITUO CHA EV - CHARGING STATION DODOMA CHAFUNGUA UKURASA MPYA KWA VYOMBO VYA USAFIRI VINAVYOTUMIA UMEME.

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amezindua rasmi kituo cha kwanza cha kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme EV Charging Station jijini Dodoma, hatua inayotajwa kuwa mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji nchini.

Kituo hicho kipya kilichopo eneo la Jamatini Dodoma kina chaja tatu, ambapo kila chaja ina uwezo wa kilowati 22.

Chaja hizo zina uwezo wa kuhudumia aina mbalimbali za vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, ikiwemo magari, bajaji na pikipiki.

Imeelezwa kuwa gari la umeme aina ya BYD SeaLion 6, likichajiwa kikamilifu, lina uwezo wa kusafiri hadi kilomita 600 kwa gharama ya takribani shilingi 30,000 za umeme, sawa na wastani wa uniti 80. Aidha, bajaji ya umeme ikiwa imejaa chaji inaweza kusafiri hadi kilomita 120, huku pikipiki ya magurudumu mawili maarufu kama bodaboda ikisafiri hadi kilomita 100 kabla ya kuhitaji kuchajiwa tena.

Katika hatua ya kuhamasisha matumizi ya kituo hicho kipya, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, ametangaza kuwa watumiaji wote wa vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme wataweza kupata huduma ya kuchaji bure bila malipo yoyote katika kituo hicho cha Dodoma.

Amesema huduma hiyo ya bure kwa mwezi mmoja kuanzia leo, Juni 11, 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha Watanzania, hususan wakazi wa Dodoma, kuendelea kuhamia katika matumizi ya teknolojia safi na rafiki kwa mazingira katika sekta ya usafirishaji.

Uzinduzi wa kituo hicho unatarajiwa kuwa chachu ya kuongezeka kwa matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme nchini, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza gharama za usafiri, matumizi ya mafuta na athari za mabadiliko ya tabianchi.