Kongamano la Kimataifa la Jotoardhi laanza kwa mafanikio Dar es Salaam
Lahusisha nchi 21 na Washiriki 800
Kuangazia Sera, fursa za masoko na uwekezaji
Kamishna Luoga asema lengo ni kuendeleza nishati ya Jotoardhi nchini
UNEP yaipongeza Tanzania kwa maandalizi
Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) limeanza kwa mafanikio
jijini Dar es Salaam ambapo Wataalam takriban 800 kutoka 21 duniani
wameshiriki.
Hayo yameelezwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi
Innocent Luoga wakati akifungua mafunzo kuhusu masuala mbalimbali ya
Jotoardhi kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt.
Khatibu Kazungu ikiwa ni sehemu ya programu ya siku saba za Kongamano
hilo.
“Katika Kongamano hili washiriki watafaidika na masuala mbalimbali
ikiwemo kupata ufahamu wa kina kuhusu maendeleo ya rasilimali za
jotoardhi kupitia mazungumzo na warsha za kiufundi, Kubadilishana
uzoefu, kutembelea na kujifunza kwa vitendo katika maeneo ya miradi ya
jotoardhi, kujadili athari za masoko ya kaboni (carbon markets) na
kukuza Uwezo: Kupitia kozi fupi za kiufundi (Pannel and Parallel
Sessions.” Amesema Mhandisi Luoga
Ameongeza kuwa, kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hilo
kunatokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini
ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uendelezaji wa Sekta ya
Nishati ikiwemo Jotoardhi.
“Ili tuweze kuwa na umeme wa uhakika na usalama wa nishati nchini
lazima umeme uzalishwe kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo Maji, Gesi,
Jua, Upepo na Jotoardhi yenyewe na lengo la Serikali ni kuachana na
utegemezi vyanzo vichache vya umeme.” Amesema Mhandisi Luoga
Ameeleza kuwa, Kongamano hilo la Kimataifa la Jotoardhi linaamsha ari
mpya katika uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania kwani litasaidia pia
kuongeza fursa za uwekezaji kwenye sekta hiyo.
Kongamano litafunguliwa na Makamu wa Rais, Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango
ambapo nchi mbalimbali duniani zinazoshirikiana na Tanzania katika
kuendeleza rasilimali ya Jotoardhi zinashiriki.
Ametanabaisha kuwa, Tanzania ina maeneo takriban 52 yaliyoainishwa kwa
ajili ya uendelezaji wa nishati ya Jotoardhi ambapo maeneo matano
tayari yanaendelezwa, ikiwemo Ngozi, Kiejo-Mbaka, Ruhoi, Natron na
Songwe.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi
Tanzania (TGDC), Mathew Mwangomba amesema Kongamano hilo linahusisha
wadau mbalimbali duniani ikiwemo watalam wa jotoardhi ambapo kongamano
litaangazia masuala mbalimbali ikiwemo masoko ya gesi ya ukaa na
upunguzaji wa gesi ya ukaa.
Ametaja Kauli mbiu ya Kongamano hilo kuwa ni, Kuharakisha Maendeleo ya
Rasilimali za Jotoardhi katika Afrika, Masoko ya Gesi ya Ukaa na
Upiunguzaji wa Gesi ya Ukaa”.
Ametaja faida za ARGeo C-10 kuwa ni pamoja na kufungua fursa
zinazotokana na jotoardhi na kuharakisha maendeleo ya nishati hiyo
Tazania hali itakayoongeza pia pato la Taifa na kuongeza kiasi cha
umeme.
Amesema katika Kongamano lililofanyika mwaka 2014 ambapo Tanzania
ilikuwa nchi mwenyeji, lilileta matokeo chanya ikiwemo uanzishwaji wa
kampuni ya Jotoardhi Tanzania, Wataalam wa Kitanzania kupata mafunzo
nje ya nchi na kuongeza mchango wa wadau wa maendeleo katika Jotoardhi
ikiwemo Japan (JICA), Iceland, New Zealand na Marekani.
Naye, Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa
Maziringira (UNEP) katika nchi za Kusini mwa Afrika, Meseret
Teklemarian ameipongeza Tanzania kwa kuandaa Kongamano hilo kwa
mafanikio makubwa.
Pia ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kulipa umuhimu mkubwa
Kongamano hilo kwani maandalizi ya Kongamano husika yameshirikisha
Watalam kutoka Sekta mbalimbali huku Watalam wengi kutoka Taasisi
mbalimbali na mashirika binafsi wakihudhuria mafunzo yanayoendelea
katka kongamano hilo.