KUTOKA KUNI HADI GESI: JANGWANI SEC NA DIAMOND PRIMARY ZAPIGA HATUA KUBWA NISHATI SAFI.
Serikali imezidi kusisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi za umma, huku Shule ya Sekondari Jangwani na Shule ya Msingi Diamond jijini Dar es Salaam zikiwa miongoni mwa Taasisi za mfano kwa utekelezaji wa ajenda hiyo muhimu ya kitaifa.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mifumo ya nishati safi Machi 26, 2026, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, alizitaka taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa siku kuachana na kuni na mkaa, na badala yake kutumia teknolojia safi za kupikia.
Alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi (2024–2034), unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
“Ninaziomba sekta binafsi ziungane na Serikali katika kufanikisha mkakati huu mkubwa wa miaka kumi, ambao tayari umeanza kuleta matokeo chanya katika taasisi mbalimbali,” alisema Luoga.
Katika ziara hiyo, alibainisha kuwa mifumo ya nishati safi hiyo imewezeshwa kupitia programu ya CookFund inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya, tayari imeanza kusambazwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mwanza. Hadi sasa, taasisi 45 zikiwemo shule, hospitali na vyuo vikuu zimefungiwa mifumo hiyo ya kisasa.
Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeingia makubaliano na taasisi za umma kama Magereza na Jeshi la Wananchi ili kuhakikisha wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mhandisi Luoga amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi yameleta manufaa makubwa, ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji, kulinda mazingira kwa kupunguza hewa ukaa, pamoja na kuboresha afya za wapishi.
Alitoa pongezi kwa Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa CookFund kwa mchango wao, akieleza kuwa juhudi zinaendelea kupanua mradi huo ili kufikia taasisi nyingi zaidi nchini.