Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Makamba afanya mazungumzo na...

​Makamba afanya mazungumzo na kampuni zitakazotekeleza mradi wa LNG

Makamba afanya mazungumzo na kampuni zitakazotekeleza mradi wa LNG

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba amekutana na Viongozi wa Kampuni zitakazotekeleza Mradi wa kuchakata na kusindika Gesi ya Asilia (LNG).

Makamba amekutana na viongozi hao ambao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Medco Energi, Roberto Lorato, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Pavilion Energy ltd, Alan Heng pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Shell nchini Tanzania, Jared Kuel kwa lengo la kujadili maendeleo ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa LNG.

Mkutano huo umefanyika Aprili 9, mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Athumani Mbuttuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania Mussa Makame na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Nishati.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Medco Energi, Roberto Lorato amesema kampuni hizo ziko tayari kuanza utekelezaji wa mradi huo mara baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Kwa upande wake, Waziri Makamba amezihakikishia kampuni hizo kuwa Serikali iko tayari kuutekeleza mradi huo Mkubwa na wa kimkakati kwa manufaa makubwa nchini.

Alifafanua kuwa mradi huo utakaogharimu zaidi ya shilingi Trilioni 70 za kitanzania ni muhimu kwa taifa katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo zaidi.

Vilevile aliwahakikishia wawekezaji kuwaSerikali imeanza maandalizi ya utekelezaji wa Mradi kwa kuanzisha Ofisi Maalum(LNG Project Office)ili kurahishisha uratibu wa masuala yote ya Mradi.