Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Makamu wa Rais atoa maelekezo...

​Makamu wa Rais atoa maelekezo mahsusi kuboresha utekelezaji wa Mradi wa Julius Nyerere (JNHPP).

Makamu wa Rais atoa maelekezo mahsusi kuboresha utekelezaji wa Mradi wa Julius Nyerere (JNHPP).

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango ametoa maelekezo mbalimbali kwa Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) yatakayoboresha utekelezaji Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ili kuweza kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Maelekezo hayo ameyatoa tarehe 13 Oktoba, 2021 wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku mbili ya kutembelea mradi wa JNHPP kilichofanyika katika eneo la Mradi na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Nishati, January Makamba.

Ameelekeza kuwa, Katibu Mkuu Kiongozi kuteua timu ya wataalam kutoka Wizara mbalimbali, baadhi ya taasisi za Serikali na vyombo vya Ulinzi na Usalama itakayochambua changamoto mbalimbali zinazohusu mradi huo na kupendekeza utatuzi wake.

“Timu ya hiyo ya Serikali ichambue changamoto hizo na kupendekeza ushauri wake, ikiwemo suala la ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka eneo la mradi hadi mji wa Chalinze na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme,” alibainisha Makamu wa Rais

Alisisitiza kuwa, TANESCO ijenge njia ya kusafirisha umeme kutoka eneo hilo la mradi kwenda Chalinze na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Chalinze ili kuwezesha majaribio ya kuzalisha umeme mara mradi utakapokamilika.

Maelekezo mengine ni pamoja na TANESCO kuwa na wataalam wa kutosha katika nyanja mbalimbali ikiwemo Wahandisi, Wanasheria, Wasanifu na Wahandisi wa mabwawa ya kufua umeme watakaowezesha Shirika hilo kufanya kazi kwa ufanisi ikiwemo ya usimamizi wa mradi huo.

“Angalieni uwezekano wa kuongeza wataalam sehemu zenye mapungufu, mkandarasi aongeze vitendea kazi vinavyohitajika, na pia muda wa kufanya kazi uangaliwe ili mradi huu ufanikiwe.” amesisitiza Makamu wa Rais.

Pia, alimuelekeza Waziri wa Nishati kufuatilia masuala yanayohusu fedha zinazotengwa kwa ajili ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ili yafanyike kwa ufanisi.

Kwa upande mwingine, ameilekeza Wizara ya Nishati, TANESCO na mkandarasi wa mradi kukutana ili kujadili namna ya kufidia muda uliopotea kutokana na sababu mbalimbali katika utekelezaji wa mradi huo.

Aliongeza kuagiza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kusaidia kuharakishwa kwa upatikanaji wa vibali vya wataalam kutoka nje ya nchi wanaoingia nchini kufanya kazi kwenye mradi huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, January Makamba alimshukuru Makamu wa Rais kwa kutembelea mradi wa JNHPP na kutoa maelekezo hayo na kuahidi kuanza kuyafanyia kazi mara moja.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria kikao hicho cha majumuisho ni pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Naibu Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigellah, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.