Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Makatibu Wakuu waridhishwa na...

​Makatibu Wakuu waridhishwa na mradi JNHPP, ujenzi wafikia 54%

Makatibu Wakuu waridhishwa na mradi JNHPP, ujenzi wafikia 54%

Zuena Msuya, Pwani

Kamati ya Uongozi ya Mradi wa Julius Nyerere inayoundwa na Makatibu Wakuu wa Wizara 15, imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali aliongoza kamati hiyo, Julai 13, 2021, wakati wa ziara ya makatibu wakuu hao ya kutembelea na kukagua mradi huo wa kufua umeme wa Megawati 2,115 kwa kutumia maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji, mkoani Pwani.

Akizungumza kwa niaba ya Makatibu wakuu hao, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu ya Rais Mazingira, Marry Maganga alisema kuwa wamefarijikakuona kasi ya utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia asilimia 54 ya ujenzi wa maeneo muhimu ya mradi.

Maganga alisema kuwa Makatibu wakuu wote wanaohusika moja kwa moja na mradi huo, wanaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kuhakikisha kila kitu kinatekelezeka kwa wakati bila kikwazo chochote ili kuhakika kuwa mradi huo utakamilika kama ulivyopangwa Mwezi Juni 2022.

“Mradi huu unatekelezwa kwa fedha zetu wenyewe watanzania,sisi makatibu wakuu tunajukumu la kuusimamia ipasavyo katika utekelezajiwake kwa kuhakikisha kuwa kila kitu kinaenda kama inavyotakiwa kurahisisha utekelezaji wa mradi huo, kwa umoja wetu tunajivunia kuwa sehemu ya kutekeleza mradi huu”, alisema Maganga.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, aliwaeleza makatibu wakuu hao kuwa, kwa kuwa Wizara ya Nishati ndiyo msimamizi mkuu wa utekelezaji wa mradi huo itahakikisha inakuwa bega kwa bega na wizara jumuishi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Aidha Mahimbali alisema kuwa wataendelea kumsimamia ipasavyo mkandarasi aliyepewa dhamana ujenzi wa mradi huo ili atekeleze majukumu yake ipasavyo kama ilivyoelekezwa katika makubaliano ya mkataba wa utekelezaji.

“Utekelezaji wa JNHPP uko katika hatua nzuri ya ujenzi katika maeneo yote makuu, ikiwamo Kingo za Bwawa husika, Tuta kuu la Bwawa, Kituo cha Kuchochea Umeme pamoja na Nyumba ya kuendeshea Mitambo ya kuzalisha umeme, mwezi Novemba mwaka huu tutaanza kujaza maji kwa ajili ya kuzalisha umeme kuanzia mwezi juni 2022,” alisema Mahimbali.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka aliwataka watanzania kuvuta subira na kuwa na imani na Serikali yao kwakuwa mradi huo unatekelezeka na utazalisha umeme kama ilivyokusudiwa.

Aliwaeleza watanzania kuwa mradi huo utakapokamilika utawezesha umeme kuwa mwingi, wa uhakika na kwa gharama nafuu, vilevile hata kuuza nje ya nchi kwa watakaohitaji.

Kamati hiyo ilitembelea na kukagua maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa Mradi huo ambayo ni Handaki la Kuchepusha Maji ya Mto, Kingo za Bwawa husika, Tuta kuu la Bwawa, Kituo cha Kuchochea Umeme pamoja na Nyumba ya kuendeshea Mitambo ya kuzalisha umeme.

Aidha walitembelea na kukagua Daraja la Kudumu, Barabara, Njia ya kupitisha maji ya kuzalisha umeme, pamoja na eneo la ufungaji wa mitambo.