Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​MAKATIBU WAKUU WASTAAFU WAPON...

​MAKATIBU WAKUU WASTAAFU WAPONGEZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE

MAKATIBU WAKUU WASTAAFU WAPONGEZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE

Katibu Mkuu Kiongozi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Katibu wa Baraza la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mha. Zena Ahmed Said amepongeza Wizara ya Nishati kwa kuwaalika Makatibu na Naibu Makatibu Wakuu Wastaafu wa Wizara kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

Mradi huo unatarajiwa kuzalisha Megawati 2,115 baada ya kukamilika na hivyo kuondoa kabisa tatizo la uhaba wa umeme nchini.

Mha. Zena ametoa kauli hiyo Jumamosi Januari 21, 2023 wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea mradi ambapo amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri ukiwemo ujenzi wa tuta kuu pamoja na njia za kupitisha maji na maeneo mengine.

Amepongeza wakandarasi, Shirika la umeme nchini (TANESCO) na msimamizi wa mradi TECU ambaye ni kampuni ya Tanzania kwa kusimamia ujenzi. Aidha, Mha. Zena ameishauri Wizara ya Nishati kuandaa kanzidata itakayosaidia kufahamu wafanyakazi wote waliohusika katika ujenzi wa mradi huo ili waweze kutumika maeneo mengine yenye miradi ya kimkakati.

“Ni matumaini yetu ikifika mwezi Juni 2024 ujenzi wa huu mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Nyerere utakuwa umekamilika kwa sababu hadi sasa mradi umefikia asilimia 80.2 na utaondoa changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini," amesema Mha. Zena.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema Makatibu Wakuu Wastaafu waliotembelea mradi huo baadhi yao walihusika katika maandalizi ya awali ya utekelezaji wa mradi walipokuwa Wizara ya Nishati na Madini au Wizara nyingine za kisekta walizokuwa wakifanyia kazi.

Mhandisi Mramba amesema kila mmoja amechangia mafanikio ya mradi huo na amewapongeza Makatibu Wakuu Wastaafu kwa kukubali mwaliko wa Wizara ya Nishati kwa kufika eneo la mradi kuona maendeleo yaliyofikiwa.

Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Utumishi, Bw. George Yambesi ambaye pia ni Katibu wa Makatibu Wakuu Wastaafu amesema viongozi wastaafu wataendelea kuwa mabalozi wa Miradi inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa JNHPP.

Ziara hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Bw. Kheri Abdul Mahimbali, Kamishina wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, Kamishina Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Bw. Edward Ishengoma pamoja na watendaji wengine wa Wizara ya Nishati na TANESCO.