MASHIRIKA BINAFSI YATAJWA KUWA NGUZO MUHIMU YA MAENDELEO YA SEKTA YA NISHATI.
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, amekutana na ujumbe kutoka mashirika binafsi ya ECOTA na Social for Change (SFC) kwa lengo la kujadili fursa zilizopo katika Sekta ya nishati Nchini na namna mashirika hayo yanavyoweza kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza sekta hiyo.
Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba, Jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Luoga amesema mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa katika Sekta ya Nishati yanatokana na juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, pamoja na ushirikiano mkubwa unaotolewa na wadau mbalimbali wakiwemo mashirika binafsi ya ndani na nje ya nchi.
“Serikali imeendelea kutambua mchango mkubwa wa mashirika binafsi katika maendeleo ya sekta ya nishati, ndiyo maana imeendelea kufungua mazingira rafiki ya uwekezaji na ushirikiano ili kuhakikisha sekta hii inakua kwa kasi na kutoa manufaa kwa wananchi”. Amesema Mhandisi Luoga
Aidha, ameeleza kuwa Wizara ya Nishati imefungua fursa mbalimbali za uwekezaji katika maeneo ya umeme, nishati jadidifu, nishati safi ya kupikia pamoja na maeneo mengine muhimu, huku akiyahimiza mashirika binafsi kutumia fursa hizo kuchangia maendeleo ya sekta hiyo nchini.
Mhandisi Luoga pia amepongeza juhudi zinazofanywa na mashirika ya ECOTA na SFC kwa kujipanga kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati jadidifu pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo katika sekta za viwanda na kilimo hususan katika mikoa ya Kusini na Kanda ya Ziwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirika la SFC, Dkt. James Juakali, ameishukuru Wizara ya Nishati kwa ushirikiano na mapokezi mazuri, akieleza kuwa mashirika binafsi yataendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza sekta ya nishati nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ECOTA, Bw. Rastone Nguma, amesema mashirika binafsi yako tayari kuendelea kuunga mkono juhudi za Wizara ya Nishati katika kuhakikisha sekta ya nishati inaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.