MAWAZIRI WA NISHATI WA TANZANIA, RWANDA NA BURUNDI WAKAGUA MRADI WA UMEME WA RUSUMO (MW 80)
Mawaziri wa Nishati kutoka nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mawaziri hao, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko leo wamefanya kikao cha ngazi ya Mawaziri na kukagua mradi wa umeme wa Rusumo utakaozalisha megawati 80 na kila nchi itapata megawati 27.
Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 30 Septemba, 2023, katika eneo la mradi, wikayani Ngara Mkoa wa Kagera, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Biteko amesema kuwa, mradi huo ni wa kihistoria na kukamilika kwa mradi huo kutapelekea ongezeko la umeme kwa nchi zote tatu.
"Leo tumewasha mashine moja ya kuzalisha umeme na mashine mbili zilizobaki zitawashwa mwezi Oktoba mwaka 2023, tunawashukuru Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Africa (AfDB) kwa kuchangia fedha zilizowezesha mradi huo kutekelezeka”. Amesema Dkt.Biteko
Amesema kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na manufaa mengi ikiwemo kuimarisha upatikanaji umeme katika mikoa ya Kagera, Geita na Kigoma na hivyo kuleta manufaa mengi ikiwemo kuchochea uwekezaji katika viwanda na kukuza uchumi wa wananchi.
Amesema kuwa, mradi huo pamoja na kuhusisha miundombinu ya kuzalisha umeme na kusafirisha umeme wa msongo wa kV220, mradi pia umehusisha kujenga miradi ya kijamii ya shilingi bilioni 25 kama vile kituo cha Afya Rusumo na Lukole ,mradi wa maji Rusumo, madarasa, mabweni na maabara katika shule za msingi na sekondari pamoja na kuendeleza wananchi katika miradi ya kilimo na ufugaji.
Kuhusu uzinduzi wa mradi huo amesema kuwa utazinduliwa mwezi Desemba mwaka ambapo inatarajiwa kuwa viongozi wakuu wa nchi zote Tatu watauzindua.