MEGAWATI 50 ZA UMEME JUA KISHAPU ZAIKOSHA KAMATI YA BUNGE
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Nishati kwa kuendelea kutekeleza mkakati wa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya nishati (Energy Mix) ukiwamo mradi wa kuzalisha umeme wa jua wenye uwezo wa megawati 50 uliopo wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga.
Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 13, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Subira Mgalu baada ya kamati kutembelea na kukagua mradi huo ambao tayari umeanza kuingiza umeme katika Gridi ya Taifa.
Mhe. Mgalu amesema mradi huo ni kielelezo cha mapinduzi makubwa yanayoendelea kufanyika katika sekta ya nishati nchini, hususan katika jitihada za kupanua wigo wa uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo mbadala kama nishati ya jua.
“Mradi huu tayari umeingiza megawati 50 katika Gridi ya Taifa, jambo linaloonesha dhamira ya Serikali ya kuwa na Energy Mix badala ya kutegemea chanzo kimoja cha uzalishaji wa umeme. Kwa sasa tuna umeme wa maji, gesi na sasa tunazidi kuongeza vyanzo vingine kama jua,” amesema Mhe. Mgalu.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme nchini, hasa katika kipindi ambacho hali ya hewa imekuwa haitabiriki na kuathiri upatikanaji wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme.
Aidha, amesema Kamati imeridhishwa na matumizi ya fedha zilizotumika katika utekelezaji wa mradi huo, ambapo megawati 50 zinazozalishwa tayari zimeunganishwa katika Gridi ya Taifa na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini.
Mhe. Mgalu pia ameitaka Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea kusimamia na kutekeleza kikamilifu maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza uzalishaji wa umeme hadi kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Awali, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo tofauti, ikiwemo mradi wa umeme wa jua wa Kishapu ulioanza kutekelezwa mwaka 2023.
Amesema mradi huo unaotumia teknolojia ya Solar Photovoltaic unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza tayari imekamilika na kuingiza megawati 50 katika Gridi ya Taifa.
Ameongeza kuwa awamu ya pili ya mradi huo inatarajiwa kuanza hivi karibuni na itazalisha megawati 100 zaidi, hatua itakayoongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, awamu ya kwanza ya mradi huo imetumia Sh. bilioni 118, huku awamu ya pili ikitarajiwa kugharimu Sh. bilioni 216.
“Katika Taifa letu hatuwezi kutegemea chanzo kimoja tu cha kuzalisha umeme. Umeme wetu mwingi unatokana na mabwawa ya maji, lakini mvua zimekuwa hazitabiriki, hivyo wakati mwingine mabwawa hukosa maji ya kutosha kwa uzalishaji,” amesema Mhe. Ndejembi.
Amesema kukamilika kwa awamu zote mbili za mradi huo kutasaidia kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini kupitia nishati ya jua na hivyo kuimarisha usalama wa nishati.