MENEJIMENTI YA WIZARA YA NISHATI YATEMBELEA MRADI WA EACOP TANGA, WAFIKIA 85% YA UTEKELEZAJI.
Menejimenti ya Wizara ya Nishati imetembelea mradi wa kimkakati wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania wa EACOP (East African Crude Oil Pipeline) leo Mei 11, 2026.
Menejimenti hiyo ikiongozwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga imepokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na kujionea ujenzi wa kituo cha kupokea, kuchakata na ujenzi wa gati la kupakia mafuta.
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amesema Wizara ya Nishati imejionea kazi nzuri inayoendelea kufanyika ambapo mradi huo unatekelezwa kwa wakati na umefikia asilimia 85 ya utekelezaji.
“Tumeridhishwa na utekelezaji wa mradi huu. Umezalisha ajira kwa Watanzania katika fani mbalimbali, pia umefungua fursa nyingi kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga moja kwa moja na Taifa kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na ushiriki wa wazawa. vile vile mradi huu umesaidia jamii kupitia ukarabati wa barabara, miradi ya maji na miradi mingine ya kijamii”. Amesema Kamishna Luoga.
Akitoa maelezo ya mradi huo, Mhandisi wa Mradi wa Kituo cha Kuhifadhi Mafuta, Mhandisi Musa Msafiri amesema utekelezaji wa upande wa matenki ya kuhifadhi mafuta umefikia asilimia 94, ambao ni ujenzi wa matenki manne yenye uwezo wa kubeba mapipa 2,000,000.
Kwa upande mwingine, Mhandisi wa Ujenzi wa gati, Fred Mahenge amesema utekelezaji wa mradi wa upande wa kituo cha kupakia na kusafirisha mafuta baharini (Jet) ni zaidi ya asilimia 90.
Mradi huu umezalisha jumla ya ajira 1,834, ambapo Watanzania wamepata asilimia 84 ya nafasi zote za ajira.
Aidha mradi huu unahusisha ujenzi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, ambapo mafuta yatapakiwa na kusafirishwa kwenda soko la dunia.