The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

MHE. SALOME AWAHIMIZA WANANCHI...

MHE. SALOME AWAHIMIZA WANANCHI CHEMBA KUUNGA MKONO MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Chemba kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira, kuboresha afya na kuongeza ufanisi wa shughuli za kijamii na kiuchumi.

Mhe. Salome amesema hayo wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, wilayani Chemba mkoani Dodoma iliyolenga kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.

“Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kinara barani Afrika katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo viongozi mbalimbali wa Afrika wanaitazama Tanzania kwa namna inavyotekeleza agenda hiyo muhimu”. Amesema Mhe. Salome

Ameeleza kuwa jitihada za Rais Samia zimepelekea asilimia 28.6 ya wananchi kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Aidha, Mhe. Salome amesema kuwa wananchi wa Chemba wana jukumu kubwa la kuendelea kutunza misitu na mazingira kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka ruzuku kwenye majiko ya gesi pamoja na majiko banifu ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kumudu matumizi ya nishati hiyo.

Pia amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yatapunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi wa kuni na mkaa, pamoja na kuwawezesha wanawake kutumia muda mwingi zaidi katika shughuli za uzalishaji mali na malezi ya familia.