MIL.900/- ZALETA MAPINDUZI YA NISHATI SAFI KWA TAASISI 45.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema zaidi ya sh. milioni 900 zimetumika kufanikisha uwekaji wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika taasisi 45 zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa siku.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mifumo hiyo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Bunge, Mhe.Salome amesema uwekezaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa vitendo wa Sera ya Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuondoa utegemezi wa kuni na mkaa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukisababisha athari hasi kwa jamii na mazingira.
Amesema taasisi hizo zimeanza kutumia teknolojia za kisasa za kupikia, zikiwemo majiko banifu, gesi ya kupikia (LPG) pamoja na nishati ya umeme, hali inayochangia kupunguza kwa kiasi kikubwa moshi unaosababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji kwa wapishi na watumiaji.
“Huu si mradi wa kawaida, bali ni hatua muhimu ya kubadilisha maisha ya watu, kulinda afya zao na kuhifadhi mazingira yetu kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” amesema.
Mhe. Salome ameongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, na kwamba ni nguzo muhimu katika kufanikisha ajenda ya maendeleo endelevu nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano kutoka Umoja wa Ulaya, Marc Stalmans, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia mbali na kulinda afya, yameanza pia kuleta matokeo chanya kiuchumi, ikiwemo kupungua kwa gharama za kupikia na muda wa kuandaa chakula.
Amesema hali hiyo inasaidia taasisi kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, hususan kwa wanafunzi.
Mradi huo umefadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia Shirika la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) chini ya mpango wa CookFund, ukiwa sehemu ya ushirikiano wa kimataifa unaolenga kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na changamoto za nishati na mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia ufadhili huo, taasisi husika zimewezeshwa kupata vifaa vya kisasa vinavyotumia nishati safi na vyenye ufanisi mkubwa katika matumizi.