Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​MKAKATI WA MATUMIZI YA NISHAT...

​MKAKATI WA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA: KUONGEZA TIJA YA KIUCHUMI NA KIJAMII

Imeelezwa kuwa Mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini umefungua milango mipya ya ajira, uwekezaji na ujasiriamali huku ukilinda mazingira na kuboresha afya za wananchi.

kupitia ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na asasi za kiraia, fursa zaidi zinajengeka na kuwafanya Watanzania hasa vijana na wanawake kunufaika na uchumi wa kijani unaokua kwa kasi na kufanya Mfumo huu endelevu kuiwekaTanzania katika nafasi nzuri ya kufikia maendeleo jumuishi na kupunguza umaskini kwa vizazi vya sasa na baadae.

Hayo yameelezwa leo Novemba 21, 2020 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mha. Advera Mwijage wakati wa kipindi cha Clouds 360 Chenye lengo la kuelimisha umma wa watanzania juu ya ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Mha.Mwijage amesema kuwa Matumizi ya nishati safi ya kupikia yamekuwa chachu muhimu katika kubadili maisha ya Watanzania wengi, hususani wale wanaoishi vijijini na miji midogo kwani mageuzi haya yanayohusisha matumizi ya gesi (LPG), majiko banifu, gesi asilia, biogas na umeme, yameleta maboresho makubwa katika afya, mazingira na uchumi ,huku yakimpunguzia Mwanamke gharama za uendeshaji kwani Serikali ipo tayari kwa sasa kumsaidia mama jikoni, kwa kupunguza madhara ya moshi jambo linaloongeza ustawi wa familia na uwezo wa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.

“Kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia kumekua na ongezeko la mahitaji ya nishati safi ya kupikia ambapo kumekua na ongezeko la fursa nyingi za ujasiriamali na ajira katika sekta ya uzalishaji na usambazaji wa vifaa vya kupikia,kwani viwanda vidogo vinavyozalisha majiko banifu vimeajiri vijana wengi, wakati biashara za kuuza na kusambaza gesi zimepanuka kutoka mijini hadi vijijini hali ambayo imeongeza mtiririko wa kipato kwa wajasiriamali na sekta binafsi, huku ikichochea ubunifu na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira”.Ameeleza Mhandisi Mwijage.

Aidha ameeleza kuwa Wakala wa Nishati vijijini (REA) imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwani wameendelea kutoa majiko banifu kwa bei ya ruzuku huku mitungi ya gesi za Kilo 6 ikiendelea kusambazwa kwa bei rahisi pamoja na kambi 26 za Magereza zimefikiwa hali inayoonesha mapokezi ya nishati safi ya kupikia ni makubwa mno kwa wananchi.

Akizungumzia mkakati wa Mawasiliano unaotekelezwa sambamba na Ule wa nishati safi ya kupikia Kaimu Mkurugenzi wa Nishati safi ya Kupikia Wizara ya Nishati Ngereja Mgejwa ameeleza kuwa Mkakati wa Mawasiliano ni injini ya kufikisha taarifa kwa Wananchi, kwani kupitia vyombo vya habari elimu imeendelea kutolewa kwa Wananchi hivyo ni imani kuwa hadi kufikia 2034 asilimia 80% ya Watanzania watakua wanatumia nishati safi ya kupikia.

Naye, Mhandisi Wa nishati safi ya kupikia Wizara ya Nishati Benezeth Kabunduguru ameeleza kuwa lengo la ziara ni kujenga uelewa kwa wananchi na Taasisi juu ya Mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia sambamba na mkakati wa Mawasiliano wa Nishati safi ya kupikia kupitia vyombo mbalimbali vya habari, pamoja na majukwaa ya wananchi ili wananchi wote nchini waweze kufikiwa na kampeni hii na hatimaye kutumia nishati safi ya kupikia.