Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Mkataba wa kwanza wa uzalisha...

​Mkataba wa kwanza wa uzalishaji umeme Jua (MW 50) wasainiwa

Mkataba wa kwanza wa uzalishaji umeme Jua (MW 50) wasainiwa

Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imesaini mkataba wa kwanza wa uzalishaji wa umeme Jua wa kiasi cha megawati 50 utakaotekelezwa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Mkataba huo umesainiwa tarehe 29 Mei, 2023 jijini Dodoma na kushuhudiwa na Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Kwa ujumla mradi huo wa umeme wa Jua ni wa megawati 150 ambapo awamu kwanza itajengwa mitambo itakayozalisha megawati 50 na awamu ya pili itajengwa mitambo ya megawati 100 kwa jumla ya shilingi bilioni 275.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nishati amesema kuwa “kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi tunaingiza umeme wa Jua katika gridi ya Taifa, nimpomgeze Rais wetu kwa kwa muongozo na uongozi ambao umepelekea nchi kuaminiwa na washirika wa maendeleo ikiwemo Shirika la Maendeleo la Ufaransa ambalo limetoa mkopo ambao utatekeleza mradi huu.”

Ameeleza kuwa, utekelezaji wa mradi huo wa Jua ni jitihada za Serikali za kuhakikisha inatengeneza mchanganyiko wa umeme wenye afya katika gridi ya Taifa ambao utatokana na vyanzo mbalimbali kama vile maji, gesi, upepo na Jua ili hata pale chanzo moja kinapotetereka, vyanzo vingine vitaendelea kuzalisha umeme.

Waziri Makamba amesema kuwa, ili kuongeza zaidi uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati jadidifu, Serikali inakuja na Sera mpya ya Nishati Jadidifu (iko kwenye maandalizi) ambayo itasaidia nchi kuongeza uwekezaji kwenye eneo hilo kwani fedha nyingi duniani, masoko ya mitaji na teknolojia mpya zinajielekeza kwenye nishati jadidifu.

Ameongeza kuwa, kwa sasa kazi inayofanyika pia ni kuainisha maeneo yaliyo na rasilimali ya nishati jadidifu na kipaumbele kitakuwa kwa wazawa kuwekeza kwenye miradi kama ya Upepo na Jua na Serikali itawaunga mkono na kwamba Serikali itakuja na muongozo wa utekelezaji wa suala hilo.

Ameongeza kuwa, kwa maeneo yaliyo nje ya gridi kama vile visiwa, bado Serikali itaendelea kuwezesha jitihada za kupelewa umeme kwa kutumia miradi ya nishati jadidifu kama vile Jua na Upepo.

Akitoa taarifa ya mradi huo wa umeme Jua, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande amesema awamu ya kwanza itajumuisha ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme kwa teknolojia ya solar photovoltaic kwa ukubwa wa megawati 50 na ujenzi wa kituo kipya cha kuongeza umeme msongo wa kilovolti 33/220 ikiwa ni pamoja na kuunganisha kituo hicho kwenye gridi ya Taifa kwa msongo wa kV 220 kwenye laini ya kutoka Singida hadi Shinyanga.

Amesema kuwa mkandarasi mjenzi wa mradi huo wa Awamu ya Kwanza ni kampuni ya Sinohydro corporation ya nchini China na Mkandarasi mshauri ni kampuni ya JV Artelia ya Ufaransa na Energiovida ya Tanzania na gharama za mradi ni shilingi Bilioni 109.

Amesema kuwa mradi huo wa awamu ya kwanza utekelezaji wake hautazidi miezi 12.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Nishati na TANESCO kwa mradi huo na ameahidi kuwa watawapa ushirikiano wakandarasi wa mradi ili watekeleza mradi huo kwa wakati na pia kuutunza ili uweze kunufaisha wananchi wa Shinyanga na Tanzania kwa ujumla.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Judith Kapinga amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya Nishati nchini

Amepongeza Wizara na TANESCO, kwa kubuni miradi mbalimbali ambayo itapelekea nchi kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kishapu, Boniphace Butondo amepongeza kwa mradi huo ambao amesema kuwa utakuwa na manufaa makubwa kwani pamoja na kupata umeme katika maeneo mbalimbali kama migodi, mradi huo utafaidisha wananchi wanaozunguka mradi kwa kupata huduma za kijamii kama shule na maji.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga.