MRADI WA GRIDI IMARA KUIMARISHA UPATIKANAJI UMEME – MHE. MWIGULU.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa utekelezaji wa Mradi wa Gridi Imara utakuwa suluhu ya upatikanaji wa umeme wa uhakika utakaokidhi ongezeko kubwa la matumizi ya umeme kufuatia upanuzi wa huduma hiyo vijijini, vitongojini, viwandani na katika maeneo ya uchimbaji.
Amesema wakati wa utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), tathmini za kitaalam zilionesha kuwa mahitaji ya umeme yatazidi kuongezeka, hali iliyomfanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuelekeza kuanza kwa utekelezaji wa Mradi wa Gridi Imara unaogharimu zaidi ya shilingi trilioni 1.1 ili kuimarisha usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini.
Mhe. Mwigulu amesema hayo Mei 17, 2026 akiwa katika ziara yake mkoani Dodoma, Wilaya ya Chemba, alipokuwa akisikiliza na kutatua kero za wananchi.
Ameongeza kuwa tayari amepata fursa ya kutembelea baadhi ya miradi ya Gridi Imara ikiwemo mradi wa Mkata mkoani Tanga ambao aliweka jiwe la msingi, akieleza kuwa mradi huo ukikamilika utaimarisha upatikanaji wa umeme katika wilaya Kilindi na Handeni mkoani humo.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuweka nguvu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (MW 2,115) ambao kwa sasa umekamilika na umeanza kuzalisha umeme uliounganishwa katika Gridi ya Taifa.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kuondoa changamoto ya upungufu wa umeme nchini, tofauti na ilivyokuwa awali.