MRADI WA KUFUNGA MIFUMO YA UMEME JUA MAENEO YA VISIWANI KWA BEI YA RUZUKU WAZINDULIWA
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amezindua mradi wa kusambaza mifumo ya umeme jua visiwani unaolenga kuweka mifumo 20,000 ya umeme jua katika visiwa 120 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 8 ambapo Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka ruzuku hadi ya asilimia 75 katika gharama za uunganishaji umeme.
Mhe. Salome Makamba amezindua mradi huo katika kisiwa cha Bezi wilayani Ilemela mkoani Mwanza ambapo mradi huo unatekelezwa chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
"Maeneo ya visiwani na delta yana changamoto za kipekee, zikiwemo umbali kutoka Gridi ya Taifa, gharama kubwa za usafirishaji wa vifaa na mtawanyiko wa makazi unaoongeza gharama za usambazaji wa nishati ya umeme. Hata hivyo, changamoto hizi haziwanyimi wananchi haki ya kupata huduma ndio maana Serikali imekuja na mpango huu mahsusi wa matumizi ya mifumo ya umeme jua pamoja na gridi ndogo kama suluhisho la haraka la kuwafikia wananchi wa visiwa na maeneo ya pembezoni." Amesema Mhe.Salome
Ameeleza kuwa hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa umeme katika maeneo kama hayo ya visiwa ni pamoja na kutoa ruzuku kwa mifumo ya umeme jua ili kuharakisha upatikanaji wa nishati safi, kupunguza utegemezi wa vyanzo visivyo endelevu kama dizeli, na kuhakikisha gharama za nishati zinakuwa nafuu.
Amesema mradi huo aliouzindua una mchango wa moja kwa moja katika kukuza Uchumi wa Buluu, ambao ni kipaumbele cha Taifa katika maeneo ya pwani na visiwa kwani mifumo ya umeme jua inayofungwa itawawezesha wavuvi kuongeza thamani ya samaki na dagaa kabla ya kupelekwa sokoni, jambo litakaloongeza mapato ya wananchi, Halmashauri pamoja na nchi, kuimarisha shughuli za ufugaji wa samaki (aquaculture), kilimo cha mwani, na huduma za utalii wa fukwe na visiwa, ambazo zote ni sehemu ya Uchumi wa Buluu.
Mhe. Salome amemshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati na kueleza kuwa Wizara itaendelea kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha ubora, uwazi na uwajibikaji vinazingatiwa katika kila hatua.
Aidha, ameiagiza REA na TANESCO kuweka mifumo ya umeme kwa taasisi zinazotoa huduma muhimu kwa jamii kama vituo vya afya, mashule, vituo vya polisi ambavyo hadi sasa bado havijapata huduma hiyo.
Vilevile ameiagiza REA kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo ya minada, stendi na masoko.Na katika kisiwa hicho cha Bezi wafanye tathmini ya matumizi ya nishati safi katika soko la samaki na kuweka miundombinu ya nishati safi ya kupikia ili kuwalinda wakaangaji na wateja dhidi ya moshi wa kuni na mkaa ambao una athari kwa afya ya binadamu na mazingira.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Mhandisi Edson Ngabo amewaasa wananchi kutumia miradi ya umeme