Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

MRADI WA KUPELEKA UMEME WA GRI...

MRADI WA KUPELEKA UMEME WA GRIDI RUKWA UMESHAANZA- MHE. KAPINGA

Asema upungufu wa umeme unazidi kupungua

Katika jitihada za kuhakikisha maeneo yote nchini yanapata umeme wa uhakika, Serikali imeshaanza kutekeleza mradi wa kupeleka umeme wa Gridi katika Mkoa wa Rukwa kupitia mradiwa TAZA ulioanza kutekelezwa mwezi Novemba, 2023 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Agosti, 2026.

Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi, Mhe. Aida Khenani aliyetaka kufahamu mkakati wa kumaliza changamoto ya upatikanaji umeme wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa.

Amesema kuwa, kwa sasa TANESCO inaendelea kufanya maboresho ya miundombinu ili kupunguza changamoto ya upatikanaji umeme mkoani humo na kujenga kituo kipya cha kupoza umeme.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme nchini amesema kuwa, upungufu wa umeme unaendelea kupungua akitaja takwimu kuwa, upungufu umepungua kutoka megawati 400hadi 144 kwa siku ya leo.

Ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbaliili kuboresha hali ya upatikanaji umeme nchini akitolea mfano utekelezaji wa Mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao inatarajiwa kuwa, katika mwezi wa Pili kuelekea Machi mwaka huu utaanza kuingiza megawati 235 katika Gridi ya Taifa.

Mhe. Kapinga pia amezungumzia kazi ya upelekaji umeme wa gridi mkoani Katavi ambapo ameeleza kuwa, tayari kuna mradi unaoendelea kutekelezwa na kwa sasa baadhi ya vituo vya kupoza umeme vimekamilika na hivyo, nguvu sasa inawekwa zaidikatika ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kwenda mkoani humo.