Mradi wa Umeme Jua Kayenze Wazalisha MW 5; Waongeza Nguvu ya Umeme na Maendeleo Ushetu
Naibu Waziri wa Nishati na Mbunge wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Salome Makamba, amesema mradi wa umeme wa jua wa Kayenze uliopo katika Jimbo la Ushetu unazalisha megawati 5 za umeme ambazo zinaingizwa katika Gridi ya Taifa kupitia njia ya msongo wa kilovolti 33 (33kV).
Mhe. Salome amesema mradi huo ulikamilika mwezi Mei mwaka 2025 na kuanza kufanya kazi mara moja, hatua iliyosaidia kuongeza upatikanaji wa umeme katika eneo hilo na maeneo ya jirani.
Mhe. Salome ameyasema hayo leo, Machi 5, 2026, wakati wa ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi, aliyefika kukagua maendeleo ya mradi huo.
Mhe. Salome ameeleza kuwa mbali na kuimarisha upatikanaji wa umeme, mradi huo pia umechangia maendeleo ya jamii kwa kujenga jengo la zahanati katika Kijiji cha Kayenze kwa gharama ya shilingi milioni 130.
Akizungumzia hali ya usambazaji wa umeme katika Jimbo la Ushetu, Mhe. Salome amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 136 vya jimbo hilo.
Ameongeza kuwa vitongoji takribani 100 vilivyosalia vinatarajiwa kufikiwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030, jambo litakalosaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo hilo